Matiang'i: Kukamatwa kwa Linturi hakukuwa na uhusiano na BBI

Muhtasari

Matiang’i aliambia kamati hiyo kwamba seneta Linturi alikamatwa ili kuhojiwa na kuandikisha taarifa kuhusiana na mashtaka 37 ya uhalifu ambayo idara ya DCI imekuwa ikifuatilia tangu mwaka 2018.

Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang'i
Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang'i Waziri wa Usalama wa ndani Fred Matiang'i

Waziri wa usalama wa ndani Fred Matiang’i amepuuzilia mbali madai kuwa kukamatwa kwa seneta wa Meru Mithika Linturi wiki iliyopita kulikuwa na uhusiano na muswada wa marekebisho ya katiba.

Matiang’i alifika mbele ya kamati ya usalama ya bunge kufuatia agizo la Spika Kenneth Lusaka kutaka idara ya usalama kueleza sababu ya kukamatwa kwa Linturi alipokuwa njiani kwenda bungeni wiki iliyopita.

Waziri alikanusha madai ya baadhi ya wanasiasa kuwa kukamatawa kwa seneta huyo kulihusiana na muswada wa marekebisho ya katiba uliyokuwa ukijadiliwa katika seneti.

Matiang’i aliambia kamati hiyo kwamba seneta Linturi alikamatwa ili kuhojiwa na kuandikisha taarifa kuhusiana na mashtaka 37 ya uhalifu ambayo idara ya DCI imekuwa ikifuatilia tangu mwaka 2018.

Habari za kukamatwa kwa Linturi ziliibua mjadala mkali katika seneti huku maseneta wakiahirisha shughuli za kawaida na vikao vyao ili kushughulikia kukamatwa kwa seneta mwenzao.

Spika Kenneth Lusaka aliagiza idara ya polisi kueleza sababu zilizopelekea Linturi  kukamatwa akiwa njiani kwenda katika majengo ya bunge ambapo hoja muhimu ya kitaifa ilikuwa tayari inajadiliwa.