Mudavadi awataka wakenya kutumia busara katika mchakato wa BBI

Muhtasari

• Mudavadi amesema kuwa ni wakati mwafaka wa wakenya kutafakari ni uongozi upi wanatarajia ifikiapo mwaka wa 2022.

Kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Picha:HISANI
Kinara wa ANC Musalia Mudavadi. Picha:HISANI

Kiongozi wa chama cha ANC Musalia Mudavadi amewataka wakenya kufanya uamuzi wa busara wakati kura ya maamuzi kuhusiana na suala zima la mchakato wa kuifanyia marekebisho katiba ya sasa kupitia mfumo wa BBI itakapoitishwa.

Akizungumza kwenyemazishi ya Mzee John Etemesi, katika eneo la Sibanga, eneo bunge la Chereng’any kaunti ya Trans Nzoiasiku ya Ijumaa, Mudavadi amesema kuwa ni wakati mwafaka wa wakenya kutafakari ni uongozi upi wanatarajia ifikiapo mwaka wa 2022.

Akiwa ashatangaza azma yake ya kuwania urais, alisema baadhi ya viongozi hasa wa kisiasa waliochaguliwa na wakenya ni wenye ubinafsi mwingi, ujanja na wenye hulka potovu hasa wasio na maono ya kuwasaidia na kuwafanyia kazi wananchi waliowatia mamlakani.

Mudavadi akigusia tajriba, urithi na ueledi wa utendakazi wa marehemu Mzee Etemesi alipohudumu kama mkuu wa mkoa wakati wa enzi za marehemu rais mstaafu Daniel Arap Moi, Kiongozi huyo wa chama cha ANC aligusia pia umuhimu wa umoja wa wakenya wote katika siku za usoni akisistiza umuhimu wa ushirikiano wa Pamoja kati ya viongozi na wakenya ili kukuza demokrasia na maendeleo.

Alikuwa Pamoja na Kiongozi wa chama cha Ford Kenya Moses Wetangula, Mawaziri Eugene Wamalwa na James Macharia Pamoja na wabunge kadhaa kutoka eneo la magharibi mwa Kenya.