Kikosi maalum cha ulinzi wa rais na naibu wake chagawanywa

Mabadiliko haya katika utaratibu wa usalama pia yameathiri walinzi wa Rais mstaafu Mwai Kibaki na familia yake

Muhtasari

• Walinzi wa rais wanaoambatanishwa na familia ya rais sasa watapokea maagizo moja kwa moja katika Ikulu ya rais.

• Walinzi wa naibu rais William Ruto wataripoti  kwenye makazi yake rasmi mtaaani Karen.

Msafara wa rais Uhuru Kenyatta
Msafara wa rais Uhuru Kenyatta
Image: MAKTABA

Taarifa ya Gideon Keter na Cyrus Ombati

 

Kikosi maalum cha ulinzi wa rais Uhuru Kenyatta na naibu rais William Ruto na familia zao kimegawanywa.

Katika hatua ambayo inaashiria kuwepo kwa tofauti kubwa kati ya viongozi hao wawili, walinzi wa rais wanaoambatanishwa na familia ya rais sasa watapokea maagizo moja kwa moja katika Ikulu ya rais.

Walinzi wa naibu rais William Ruto wataripoti  kwenye makazi yake rasmi mtaaani Karen.

Walinzi wa rais na naibu wake , tangu wachukuwe mamlaka ya uongozi mwaka 2013, wamekuwa wakifanya kazi kama kitengo kimoja na wamekuwa wakitumwa kushika doria bila kujali kwa viongozi hao wawili na familia zao.

Mabadiliko haya katika utaratibu wa usalama pia yameathiri walinzi wa Rais mstaafu Mwai Kibaki na familia yake.

Duru kadhaa ndani ya ofisi ya rais ziliambia Star kwamba hatua hiyo iliafikiwa kutokana na uchachu wa uhusiano baina ya Uhuru na Ruto.

Wengine walisema mabadiliko hayo yanalenga kudhibiti kuenea kwa virusi vya Covid-19 kati ya ofisi hizo mbili.

Ruto hivi karibuni amekuwa akihutubia mikutano mikubwa ya hadhara kote nchini na walinzi wana jukumu la kudhibiti umati, hali inayowaweka waweka katika hatari kubwa ya kuambukizwa.

Uhuruto
Uhuruto

“Mabadiliko hayo yameanza kutumika hivi karibuni. Utaratibu huo unatumika hadi hapo agizo la kubatilisha litakapotolewa tena, ”afisa aliyeoomba kutotajwa jina kwa kuhofia hatua za kinidhamu aliambia Star.

Inspekta mkuu wa Polisi Hilary Mutyambai alikataa kuzungumzia mabadiliko hayo.

"Hatuwezi kujadili hilo. Usalama wa Rais, DP na VIP wengine hauwezi kujadiliwa hadharani tafadhali, "aliiambia Star kwa simu.

Uhusiano kati ya Rais Kenyatta na naibu rais Ruto na washirika wao umekuwa ukizorota tangu 2018. Katika kipindi hicho, Ruto tayari alikuwa ameelezea hofu kuhusu maisha yake.

Mwezi Juni mwaka jana, mawaziri kutoka Mlima Kenya waliagizwa kufika katika makao maku ya DCI kuhusu madai ya kuwepo kwa njama ya kumuua Ruto.

Ruto mwenyewe alilalamika kwa DCI kwamba njama hiyo ilipangwa katika Hoteli ya La Mada na maafisa wakuu wa serikali.

Mwezi Septemba mwaka jana, walinzi wa rais walikamatwa nyumbani kwa mbunge wa Kapseret Oscar Sudi alipojaribu kukwepa agizo la kukamatwa kwake.

Kikosi cha ulinzi wa rais kina takriban maafisa 200. Kikosi hicho chenye maafisa wenye tajiriba kuu hutolewa kutoka kitengo cha Recce na G-Company.

Kamanda wao ni afisa mwandamizi wa kiwango cha Msaidizi wa Inspekta mkuu wa polisi.

Kamanda wa zamani wa Kampuni ya Recce Josephat Mbuthia Kirimi ndiye kamanda wa sasa wa PEU. Amekuwa katika nafasi hiyo tangu 2018 alipochukua nafasi ya Naibu Inspekta Jenerali wa Polisi wa sasa Edward Mbugua.