Keegan Oyugi, Mkenya aliyetoweka Minnesota, Marekani wiki mbili zilizopita apatikana akiwa ameaga

Mwili wake ulipatikana ndani ya gari lake

Muhtasari

•Keegan Oyugi, 26, alipatikana akiwa ameaga ndani ya gari lililokuwa limehusika kwenye ajali maeneo ya South Metro.

•Polisi hao wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na ajali iliyotokea na mchunguzi wa kidaktari kutoka Hennepin atakamilisha uchunguzi wa mwili hivi karibuni.

Keenan Oyugi
Keenan Oyugi
Image: Hisani

Mwili wa raia wa Kenya ambaye alitoweka wiki mbili zilizopita huko Minessota, Marekani  umepatikana.

Keegan Oyugi, 26, alipatikana akiwa ameaga ndani ya gari lililokuwa limehusika kwenye ajali maeneo ya South Metro.

Maafisa wa polisi eneo la Minnesota walisema kuwa gari ambalo lilipatikana kando ya barabara kuu ya Highway 101 upande wa Savage  lilikuwa la Oyugi. Walisema kuwa mwili wake ulipatikana ukiwa umefungwa  kwa mshipi kwenye kiti cha gari hiyo.

"Tunaposubiri matokeo ya uchunguzi wa daktari, fikra na mawazo na maombi yetu yanaenda kwa familia ya Oyugi" polisi walisema.

Polisi hao wanaendelea na uchunguzi kuhusiana na ajali iliyotokea na mchunguzi wa kidaktari kutoka Hennepin atakamilisha uchunguzi wa mwili hivi karibuni.

Kulingana na Minesota News barabara ambazo zinaelekea magharibi kwenye barabara kuu iliyo upande wa South Metro zilifungwa baada ya mtu kupiga ripoti kuwa alikuwa ameona gari nyekundu lililokuwa limegongwa vibaya likiwa kwenye kichaka kidogo.

Kabla ya kutoweka kwake, Mshale News walikuwa wameripoti kuwa Oyugi alikuwa ametumia ndugu yake mdogo ujumbe akisema kuwa anaelekea nyumbani pande za St. Bonifacius kutoka maeneo ya ziwa la Prior. Hata hivyo, Oyugi hakufika nyumbani.

Oyugi alikuwa amehitimu kutoka shule ya upili ya Wichita Southeast High  School na akaanza kucheza mpira wa vikapu  katika maeneo ya Kansas.

(Utafsiri; Samuel Maina)