Mauaji: walinzi wanne wauawa Siranga, Siaya

Muhtasari

Walinzi hao wanne waliuawa na majambazi waliovamia soko la Siranga usiku wa Jumapili.

Pingu
Image: Radio Jambo

NA DICKENS WASONGA 

Huzuni ilitanda katika eneo la Siranga katika kaunti ya Siaya baada ya walinzi wanne kuuawa na watu wanaoshukiwa kuwa majambazi.

Walinzi hao wanne waliuawa na majambazi waliovamia soko la Siranga usiku wa Jumapili.

 Polisi walisema majambazi hao pia waliiba mali ya thamani isiyojulikana kutoka kwa maduka ndani ya kituo hicho cha kibiashara.

Kamanda wa polisi wa kaunti ya Siaya Michael Muchiri alithibitisha shambulio hilo na kuongeza kuwa Uchunguzi ulikuwa umezinduliwa.

Muchiri alisema kuwa vikosi mbali mbali vya usalama, vikiongozwa na afisa wa Upelelezi wa jinai kaunti ya Siaya wametumwa eneo la tukio kubaini ni nini hasa kilitokea.

Taharuki ilishuhudiwa katika soko hilo siku ya Jumatatu asubuhi baada ya wakazi kuzuia polisi kuchukua miili ya wahasiriwa, wakiwatuhumu maafisa wa usalama walio katika kituo cha polisi cha Siranga kwa ulegevu.