Uhuru amdhubutu Ruto kujiuzulu

Sijui nini kimetokea isipokuwa ukweli ni kwamba anajaribu kujenga ngome yake ya kisiasa

Muhtasari

• Rais alisema hakuwa na ufahamu wowote kwa nini upande wa DP Ruto umechagua mashambulio dhidi ya utawala wake.

• Rais alihimiza utulivu akisema hatua yake ya kuiunganisha nchi haimaanishi kupunguza nafasi za mtu yeyote kumrithi.

Rais Kenyatta (kushoto) na naibu wake Ruto (kulia) walikuwa wakiitwa mapacha, kutokana na 'uswahiba wao kwenye chaguzi zilizopita kupitia Jubilee
Rais Kenyatta (kushoto) na naibu wake Ruto (kulia) walikuwa wakiitwa mapacha, kutokana na 'uswahiba wao kwenye chaguzi zilizopita kupitia Jubilee
Image: GETTY IMAGES

Uhusiano baina ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto sasa unaonekana kuzorota hata zaidi baada rais Kenyatta kumthubutu naibu wake kuondoka serikali badala ya kuidhalilisha kutoka ndani.

Akizungumza na wahariri siku ya Jumatatu , rais hakuficha kukasirishwa kwake na ukosoaji uliotolewa dhidi ya utawala wake na kambi ya Ruto .

Rais alisema hakuwa na ufahamu wowote kwa nini upande wa DP Ruto umechagua mashambulio dhidi ya utawala wake.

Aliwaambia waandishi wa habari jijini Nairobi kwamba hakuwa na shida na Ruto kujenga ngome yake kisiasa lakini alihoji njia ambazo timu ya UDA inatumia. UDA ni chama kipya kinachoungwa mkono na naibu wa rais .

"Sijui nini kimetokea isipokuwa ukweli ni kwamba anajaribu kujenga ngome yake ya kisiasa . Ninahisi ni bahati mbaya jinsi anavyofanya.. ni vibaya," rais alisema.

Uhuru aliongeza kuwa alishangaa kwanini naibu wake alikuwa akipinga mchakato wa BBI akisema "maswala yaliyopelekea kuundwa kwa BBI ndio yaleyale yaliyowaleta pamoja".

"Ikiwa ninataka sasa kupanua hilo, kuna shida? Tukirudi nyuma hadi mwaka wa 2013 imekuwa ajenda yangu ya kuleta watu pamoja," Uhuru alisema. "Ikiwa mgawanyiko wa 2007 ulituleta pamoja, kuna shida tukiwaleta watu wengine ndani?" alihoji

Hatua ya Rais Kenyatta (kushoto) na aliyekuwa hasimu wake Odinga (Kulia) kupeana mikono, kumekuwa mwanzo wa mtikisiko wa siasa za Ruto kwenye Ikulu
Hatua ya Rais Kenyatta (kushoto) na aliyekuwa hasimu wake Odinga (Kulia) kupeana mikono, kumekuwa mwanzo wa mtikisiko wa siasa za Ruto kwenye Ikulu
Image: GETTY IMAGES

Rais alihimiza utulivu akisema hatua yake ya kuiunganisha nchi haimaanishi kupunguza nafasi za mtu yeyote kumrithi.

"Haikunyimii nafasi zako Sio Uhuru anayechagua, ni Wakenya."

Alijutia pia kwamba maswala kadhaa yaliyosababisha mgawanyiko ambao umetikisa utawala wake yanatokana na ari yake ya kuleta umoja .

"Kuna shida gani ikiwa tuna hali ya kila mtu kujumuishwa ...ambayo haijalishi ni nani atashinda, hakuna Mkenya aliyepoteza?" Aliuliza.

 

Mchakato wa kurekebisha katiba wa BBI ulionekana kujenga mgawanyiko hata Zaidi kati ya Rais Uhuru Kenyatta na naibu wake Ruto ambao walishinda uchaguzi mara mbili wakigombea kwa tiketi moja .

Kwa mujibu wa katiba ya sasa rais hawezi kumfuta kazi naibu wake.Hatua hiyo ndio inayosababisha rais kuonekana kumtaka Ruto kuondoka serikalini badala ya kuikosoa akiwa ndani .

Licha ya kuendelea na kampeini zake za kuchaguliwa kama rais mwaka ujao ,Ruto amekuwa akieleza mafanikio ya serikali ya Jubilee huku wakati mwingine akikosoa baadhi ya sera na maamuzi yanayofanywa na serikali .

Ruto (kushoto) na Odinga (kulia), walikuwa 'maswahiba' wanaotarajia kusigana katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022
Ruto (kushoto) na Odinga (kulia), walikuwa 'maswahiba' wanaotarajia kusigana katika uchaguzi mkuu ujao wa mwaka 2022
Image: GOOGLE

Miongoni mwa mambo ambayo Ruto hakupendezwa nayo serikalini ni mchakato huo wa BBI na ushirikiano wa karibu wa rais Kenyatta na viongozi wa upinzani hasa kiongozi wa ODM Raila Odinga .

Rais pia alisema hakukubaliana na uamuzi wa mahakama ya rufaa kutupilia mbali kesi ya BBI lakini alisema ataheshimu uamuzi huo .Ruto au upande wake haujasema lolote kuhusu tamko hilo la rais kumtaka aondoke serikalini .