CEO wa Keroche Breweries Tabitha Karanja alenga kuingia seneti 2022

Muhtasari

•Hata hivyo amesema bado hajafanya maamuzi kuhusu chama ambacho atatumia kuwania kiti hicho huku akiahidi kutangaza baada ya kujadiliana na kupata ushauri kutoka kwa watu.

Tabitha-Karanja
Tabitha-Karanja
Image: HISANI

Mfanyibiashara tajika Tabitha Karanja ametangaza rasmi azma yake kuwania kiti cha useneta katika kaunti ya Nakuru.

Alipokuwa kwenye mahojiano na Standard, mkurugenzi mtendaji huyo wa Keroche Breweries alisema angependa kutumia maarifa yake ya kibiashara katika siasa.

Anasema iwapo atakabidhiwa nafasi hiyo ataangazia zaidi kilimo-biashara huku akiahidi kutengenezea wakazi wa Nakuru ajira na kumaliza umaskini.

"Sababu kubwa nataka kujiunga na siasa ni kwa sababu, watu ambao tuko katika sekta binafsi tunajulikana kutopenda siasa. Sisi ndio bado hulalamika mara kwa mara. Nahisi ni wakati mzuri sisi watu waliko kwenye sekta binafsi, watu ambao wametengeneza vitu ambavyo vinaonekana  tutokee na tutumie uongozi na usimamizi ule kwa kaunti. Tuichukue kama mtoto na tuipeleke katika hatua nyingine" Alisema Tabitha.

Hata hivyo amesema bado hajafanya maamuzi kuhusu chama ambacho atatumia kuwania kiti hicho huku akiahidi kutangaza baada ya kujadiliana na kupata ushauri kutoka kwa watu mbalimbali.

Tabitha analenga kumbwaga chini mwandani wa naibu rais William Ruto, Bi. Susan Kihika ambaye amekalia kiti hicho kwa sasa.