"Amri za mahakama sharti zizingatiwe!" Miguna Miguna atoa sababu za kukataa kujaza fomu za kurejesha uraia wake

Muhtasari

•Miguna amedai waziri wa usalama Fred Matiang'i, P.S Karanja Kibicho na wakili mkuu Ken Ogeto wanamtaka ajisajili tena ili akubalike tena kama raia wa Kenya.

•Miguna Miguna amedai hana pasipoti yake ya Kenya kwani  ilichukuliwa na kuharibiwa wakati nyumba yake ilivamiwa kabla ya kufurushwa kutoka nchini.

•Wakili huyo  ameitaka serikali itii amri ya mahakama iliyoagiza aondolewe vikwazo na kuruhusiwa  kurejea nchini huku akiwasuta wanaomwagiza ajaze fomu.

Image: TWITTER// MIGUNA MIGUNA

Wakili na mwanasiasa aliyefurishwa Kenya takriban miaka minne iliyopita amesisitiza kuwa hatajaza fomu za kurejesha uraia wake.

Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Miguna amedai waziri wa usalama Fred Matiang'i, P.S Karanja Kibicho na wakili mkuu Ken Ogeto wanamtaka ajisajili tena ili akubalike tena kama raia wa Kenya.

Hata hivyo mshauri huyo wa zamani wa Raila Odinga ameapa hatafanya kama anavyotakiwa kwani hakuwahi poteza uraia wake. 

Miguna Miguna amedai hana pasipoti yake ya Kenya kwani  ilichukuliwa na kuharibiwa wakati nyumba yake ilivamiwa kabla ya kufurushwa kutoka nchini.

"Wakati nyumba yangu iliharibiwa kwa vilipuzi, nikatekwa nyara kinyume na sheria na wakachukua pasipoti yangu halali ya Kenya nilikuwa naishi na kufanya kazi Kenya kama Wakenya wengine. Sasa wanataka "thibitisho". Kile Fred Matiang'i, Karanja Kibicho, Ken Ogeto na wenzao wanataka ni "nijaze form kupata tena uraia wangu" ambao sikuwahi poteza" Miguna amesema.

Miguna ambaye hajakanyanga ardhi ya Kenya tangu 2018 amedai kile ambacho serikali inamtaka afanye ni mtego huku akisisitiza hatakubali kunaswa.

Wakili huyo  ameitaka serikali itii amri ya mahakama iliyoagiza aondolewe vikwazo na kuruhusiwa  kurejea nchini huku akiwasuta wanaomwagiza ajaze fomu.

"Mimi kamwe huwa sikubali kuanguka katika mitego. Ni kukata tamaa, woga, ulafi na upumbavu ambao humfanya mtu aanguke kwenye mitego mibaya ya Matiang'i. Uzuri, siathiriki na uovu huo. Sitikisiki na nimemakinika kama boriti ya leza!" Miguna amesema.