Ndugu wawili wakamatwa kwa kupachika wanafamilia wadogo ujauzito

Muhtasari

•Ndugu hao wawili kutoka  kijiji cha Kanyamenda wanashukiwa kuhusika na mimba za wasichana hao, ambao wote ni wanafunzi wa shule moja ya msingi pale.

•Wasichana hao, mmoja wa darasa la nne mwenye umri wa miaka 12, na mwingine wa darasa la pili mwenye umri wa miaka 10  wana ujauzito wa wiki 20 na 11 mtawalia, kulingana na Ripoti ya daktari.

Pingu
Image: Radio Jambo

Polisi katika Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Kusini wamewakamata ndugu wawili baada ya wasichana wawili wa umri wa chini kupatikana na ujauzito.

 Ndugu hao wawili kutoka  kijiji cha Kanyamenda wanashukiwa kuhusika na mimba za wasichana hao, ambao wote ni wanafunzi wa shule moja ya msingi pale.

Wasichana hao, mmoja wa darasa la nne mwenye umri wa miaka 12, na mwingine wa darasa la pili mwenye umri wa miaka 10  wana ujauzito wa wiki 20 na 11 mtawalia, kulingana na Ripoti ya daktari.

Mmoja wa washukiwa hao, Foset Onyango Ouma, mwenye umri wa miaka 36, ​​ni baba wa mwanafunzi huyo wa darasa la nne mwenye umri wa miaka 12.

 Mshukiwa mwingine, Isaac Otieno Onyango, mwenye umri wa miaka 35 ni shemeji wa msichana wa miaka 10 wa darasa la pili.

 Chifu wa eneo la Kamak Mashariki, Jacob Opecho, alisema walifikiwa na taarifa kuhusu wasichana hao walipokuwa wakifuatilia kisa cha wizi katika kijiji jirani na nyumba ya wasichana hao, na mara moja wakaripoti kisa hicho kwa polisi.

 "Baada ya kupata taarifa hizo, maafisa kutoka kituo cha polisi cha Oyugis walivamia nyumba ya wasichana hao," alisema Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Rachuonyo Kusini, Lilies Wachira.

 Kamanda alisema wasichana hao walihojiwa na baadae ikabainika wanafamilia wa karibu walikuwa wamehusika. Washukiwa hao wamekamatwa na watafikishwa mahakamani leo, Ijumaa.

 Alisema kwa usaidizi wa Idara ya Watoto, watoto hao pia wameokolewa na kuwekwa katika shirika la kuwasaidia watoto katika Kaunti Ndogo kwa kuwa wanahitaji matunzo na ulinzi.

(Utafsiri: Samuel Maina)