Wazazi waandamana baada ya mwalimu kupachika wanafunzi 6 ujauzito Kisii

Muhtasari

•Takriban wanafunzi sita wana ujauzito kwa sasa, wengi wao wakiwa watahiniwa wa mtihani wa kitaifa wa KCPE.

•Wanafunzi walioathirika walifunguka na  kusema mwalimu huyo amekuwa akiwadhulumu kingono wakati wa masomo ya ziada siku za wikendi.

Wazazi katika shule ya msingi ya Nyarenda Public Primary iliyoko Bomachoge Chache wakizungumza na wanahabari Jumapili, Januari 30, 2022.
Wazazi katika shule ya msingi ya Nyarenda Public Primary iliyoko Bomachoge Chache wakizungumza na wanahabari Jumapili, Januari 30, 2022.
Image: MAGATI OBEBO

Mwalimu mmoja wa shule ya msingi ya Nyarenda iliyo katika eneo bunge la Bomachoge, kaunti ya Kisii amenyooshewa kidole kuhusiana na visa vya ujauzito vilivyoshamiri shuleni humo.

Takriban wanafunzi sita wana ujauzito kwa sasa, wengi wao wakiwa watahiniwa wa mtihani wa kitaifa wa KCPE.

Siku ya Jumapili, wazazi katika shule hiyo waliarifu wanahabari wangetaka mwalimu huyo akamatwe na afunguliwe mashtaka.

Walisema wanafunzi walioathirika walifunguka na  kusema mwalimu huyo amekuwa akiwadhulumu kingono wakati wa masomo ya ziada siku za wikendi.

Wanaharakati wa masuala ya kijinsia  wametilia jambo hilo maanani, wakiiomba serikali kuanza "uchunguzi wa haraka, wa kina na madhubuti kuhusu tukio hilo".

Mwanafunzi mmoja aliambia waandishi wa habari kwamba mwalimu huyo alimshawishi kuingia ofisini na kumnajisi mara kwa mara. Kwa sasa ana ujauzito wa miezi sita.

“Tumesikitika sana, tulikuwa na matumaini makubwa na mwalimu huyo lakini amegeuka mnyama. Kibaya zaidi maafisa wa wizara ambao walifahamishwa zaidi ya mwezi mmoja uliopita hawasaidii,” alisema John Kebaso, mmoja wa wazazi.

Mzazi huyo alisema visa vya ujauzito vilianza kuripotiwa mara tu baada ya mwalimu huyo kujiunga na shule hiyo.

"Hata kama hatumuhusishi moja kwa moja na visa vyote vya ujauzito, tunashuku kuwa kuna kitu kinaendelea ambacho kinahitaji kuangaziwa," mzazi mmoja alisema.

Mwanaharakati Cyrus Ogega alizungumzia uozo katika shule hiyo alipoitembelea.

“Kama wakazi tunafahamu kuna njama za baadhi ya wazazi na maafisa wa elimu katika maeneo ya Ogembo na Kenyenya kutaka suala hilo linyamazishwe ili mwalimu huyo anayekaribia kustaafu apewe pensheni yake. Hatuwezi kunyamaza kwani mwindaji anaharibu maisha ya watoto wetu, haki lazima itendeke,” mwanaharakati huyo alisema.

Pia alimshutumu mkurugenzi wa elimu wa kaunti ya Kisii Pius Ng’oma kwa kuzembea kazini, akisema anafaa kuchunguzwa pia ili kubaini uwezekano wa kuficha maovu kama hayo katika kaunti hiyo.

Ng’oma hata hivyo alisema alipigiwa simu tu na mtu lakini bado hajapokea malalamishi yoyote rasmi.

"Ninaanza uchunguzi Jumatatu. Ikithibitishwa kuwa ni kweli sheria itachukua mkondo wake,” alisema kwa  simu.

Ogega pia anamtaka mbunge wa eneo hilo Alfa Miruka kufuatilia suala hilo ili kuhakikisha wanafunzi zaidi hawadhulumiwa kingono na walimu wanaotumwa katika eneo bunge hilo.

Alisema mwalimu huyo ana historia ya kunajisi wanafunzi katika shule yake ya awali na hapaswi kuruhusiwa kufundisha katika shule yoyote nyingine nchini.

‘’Sheria iko wazi kabisa kwamba hakuna mwalimu anayewadhulumu wanafunzi kijinsia aruhusiwe darasani na huyu hatakiwi kuwa ubaguzi. Hatutafuti uhamisho bali kuzuiwa na kukamatwa ili haki ipatikane,” alisema.

Pia alitoa wito wa kuhamishwa kwa mwalimu mwingine yeyote ambaye alisaidia katika kuficha.