Msitumie jina langu kwenye kampeni zenu - Mary Kilobi

Muhtasari

• Mkewe Francis Atwoli, Mary Kilobi amewasuta vikali wanasiasa wa mrengo wa naibu rais William Ruto kwa kutaja jina lake katika kampeni zao.

• Aidha mtangazaji huyo amewaambia wanasiasa hao kujikita katika kuuza sera zao kwa wakenya badala ya kutumia jina lake vibaya licha ya kwamba yeye si mwanasiasa.

Image: HISANI

Mkewe Francis Atwoli, Mary Kilobi amewasuta vikali wanasiasa wa mrengo wa naibu rais William Ruto kwa kutaja jina lake katika kampeni zao.

Kupitia taarifa aliochapisha Jumatano 9/2/2022 katika ukurasa wake wa Instagram, Kilobi aliwaambia wanasiasa hao hasahasa wa chama cha UDA kukoma kutumia jina lake vibaya katika shughuli zao za kujitafutia kura.

“Inashangaza kwamba baadhi ya wanasiasa kwa mfano kina Rashid Echesa na Didmus Barasa wamefanya mazoea ya kutumia jina langu [KILOBI] kama kipengele cha manifesto yao katika kampeni zao,” Kilobi aliandika.

Kilobi ameonekana kukasirishwa sana na wanasiasa hao ambao wanamtumia kama daraja la kumkabili mumewe, Atwoli ambaye ameonekana kupiga mawe upande wa UDA akisema kwamba hawawezi kushinda uchaguzi mkuu wa mwezi Agosti mwaka huu.

Aidha mtangazaji huyo amewaambia wanasiasa hao kujikita katika kuuza sera zao kwa wakenya badala ya kutumia jina lake vibaya licha ya kwamba yeye si mwanasiasa.

“Wakenya wanataka sana kusikia sera zenu kwao, kumbe hamna sera? Uza sera wadau achana na Kilobi. Mimi sio mwanasiasa na wala sina mipango hiyo,” Kilobi aliandika.

Kampeni za UDA katika sehemu ya magharibi mwa Kenya zilisheheni kejeli kwa Atwoli ambaye Jumatatu alisema kwamba Ruto hatafanikiwa kuwa rais wa taifa hili, matamshi yaliyopelekea viongozi hao kutoa cheche wakiwa katika kampeni huko, Kakamega, Bungoma na Trans Nzoia.