Rafiki ya ndugu wawili waliouawa Kianjokoma asimulia yaliyojiri usiku wa mauaji

Muhtasari

•Njeru alisimulia jinsi Benson na Emmanuel walivyoonekana wachangamfu walipokuwa nao katika Klabu ya Mwamuri lakini akasisitiza hawakunywa pombe yoyote.

•Upande wa mashtaka, katika maelezo yao ya ufunguzi, ulisema watathibitisha mahakamani kwamba maafisa hao sita walipanga mauaji ya ndugu hao wawili.

Mandugu wawili wanaodaiwa kufariki mikononi mwa maafisa wa polisi
Mandugu wawili wanaodaiwa kufariki mikononi mwa maafisa wa polisi
Image: HISANI

Siku ya Jumatano rafiki wa utotoni wa ndugu wawili kutoka Kianjokoma, Embu ambao waliuawa mwaka jana alisimulia mahakama matukio ya mwisho kabla ya kufa kwao.

John Njeru alikuwa shahidi wa kwanza kusikizwa na mahakama katika kesi ya mauaji dhidi ya maafisa sita wa polisi wanaodaiwa kuwaua Emmanuel Ndwiga na Benson Ndwiga.

Maafisa walioshtakiwa ni pamoja na Benson Mputhia, Consolata Kariuki, Nicholas Cheruyoit, Martin Wanyama, Lilian Chemuna na James Mwaniki.

Njeru aliambia mahakama kuwa mnamo Agosti 1 mwaka jana, alikuwa katika duka la michezo ya video (PS) katika eneo la Kianjokoma wakati Benson alipompigia simu, akiuliza kama wangeweza kukutana kwa kuwa alitaka kumwambia jambo fulani.

Alisema kwamba wakati huo  alikuwa na rafiki mwingine kwa jina Chris Dan. Baadae Benson na Emmanuel walikutana nao nje ya duka hilo baada ya kufunga duka la nyama ya nguruwe.

"Tulikuwa sisi wanne. Tulipitia mji wa Kianjokoma kisha nikapendekeza twende tupige maji lakini ndugu hao wawili wakakataa, wakisema hawataki hangover,” Njeru alisema.

Aliendelea kusimulia jinsi Benson na Emmanuel walivyoonekana wachangamfu walipokuwa nao katika Klabu ya Mwamuri lakini hawakunywa pombe yoyote.

“Mwendo wa saa tatu na dakika 17 usiku Ben alisema kwamba masaa yalikuwa yameenda sana na hata mama yao akawapigia simu. Tuliondoka mahali hapo mwendo wa saa nne na dakika moja usiku,” alisema.

Walitumia barabara ya nyuma kuondoka klabuni na ndipo walipoona gari la polisi na  mtu mmoja aliyekuwa amevalia mavazi ya kiraia akiwa amesimama nje ya gari hilo huku mwingine akiwa ameshika fimbo kubwa.

Benson alipendekeza wakimbie wote. Walianza kukimbia lakini kwa bahati mbaya Emmanuel alijikwaa na kuanguka.

Aliongeza kuwa, "Ben alimwambia [Emmanuel] aendelee kukimbia. Alisema achana na viatu wewe hepa ."

Waliendelea kukimbia kwa sekunde kadhaa kabla Ben kusimama na kurudi pale kaka yake alipokuwa ameanguka.

Njeru alisema alipata mahali pa kujificha kwenye mtaro kwa kuwa watu wawili ambao waliona wakiwa wamesimama karibu na gari la polisi walikuwa wanawafuata.

Aliiambia mahakama kuwa alisikia sauti kama ya mtu alikuwa anapigwa na akafikiri ni Ben anavamiwa na.Alipochungulia alimwona akiwekwa ndani ya gari la polisi.

Baada ya gari kuondoka, aliona njia nyingine ya kuelekea nyumbani lakini hakuweza kuwapata Emmanuel na Benson kwa simu zao kwani zilikuwa zimezimwa.

“Siku iliyofuata nilipata missed calls za baba yao na nikampigia tena. Alikuwa anauliza kama bado niko na Benson na Emmanuel."

Njeru alimsimulia yaliyojiri usiku huo. Baba ya marehemu alimtaka aende kuwatafuta na kumtaarifu kuhusu mahali walipo.

“Nilimpigia simu Chris Dan tukutane ili tuanze kuwatafuta. Tulienda katika mji wa Kianjakoma tukiwauliza watu kuhusu mahali Land Cruiser ya polisi ilikuwa imetoka lakini hakuna mtu aliyeiona,” alisema.

Njeru alisema kuwa kwa kipindi fulani walifikiria kwenda katika mahakama ya Embu ili kuuliza ikiwa wameshtakiwa kwa kukiuka amri ya kutotoka nje, lakini baba ya Emmanuel na Benson aliwafahamisha kuwa hakuna rekodi katika kituo cha polisi cha Manyatta kuhusu wawili hao.

"Tulipanga na Chris kwenda Embu kuwatafuta lakini tulipofika katika mji wa Kianjakoma tulipatwa na uvumi kwamba marafiki zetu walikuwa wamefariki," Njeru alisema.

Njeru alimweleza wakili Danstan Omari anayewakilisha washtakiwa sita kwamba ndugu hao wawili hawakunywa pombe yoyote. Njeru, hata hivyo, alikiri kunywa glasi moja ya Keg na Chris Dan.

Alipoulizwa kwa nini hakuenda nyumbani kwa marafiki zake usiku huo au kuwapigia simu wazazi wao simu kuwafahamisha kilichotokea, Njeru alisema hakujua kuwa jambo baya lingetokea.

Mapema siku hiyo, upande wa mashtaka, katika maelezo yao ya ufunguzi, ulisema watathibitisha mahakamani kwamba maafisa hao sita walipanga mauaji ya ndugu hao wawili.

"Upande wa mashtaka utathibitisha kwamba polisi walikuwa na nia na fursa ya kuwaua watu wawili waliokufa," mahakama ilisikiza.

Upande wa mashtaka ulisema mauaji ya ndugu hao yalipangwa na kutekelezwa kwa pamoja na maafisa wote sita. Walisema watatoa ushahidi wa mashahidi kutoa maelezo ya kile kilichotokea kabla ya kukamatwa kwa ndugu wawili waliofariki.