Hakimu Brian Khaemba akataa nafasi ya JSC, ajitosa kwenye siasa

Muhtasari

• Aliyekuwa hakimu katika mahakama ya Kiambu, Brian Khaemba amesema hatarejelea majukumu yake ya uhakimu licha ya mahakama ya rufaa kumtaka arejelee majukumu yake.

• Khaemba baadaye alikubaliana na tume ya utumushi wa mahakama kumlipa mshahara wake wa kutoka 14/6/2019 hadi 31/12/2021.

Wakili aishangaza mahakama kwa ujumbe wa WhatsApp kutoka kwa mwanamke 'aliyekufa' katika kesi ya mauaji
Image: Annette Wambulwa

Aliyekuwa hakimu katika mahakama ya Kiambu, Brian Khaemba amesema hatarejelea majukumu yake ya uhakimu licha ya mahakama ya rufaa kumtaka arejelee majukumu yake.

Khaemba alipigwa marufuku baada ya kumuachilia kwa dhamana aliyekuwa gavana wa kaunti ya Kiambu, Ferdinand Waititu, huku benchi la majaji watatu liliamuru kwamba hakimu huyo arejee kazini .

Hakimu huyo alisimamishwa kazi mnamo 19/6/2019 na aliyekuwa jaji mkuu, David Maraga kwa kile alikitaja kuwa utovu wa nidhamu.

 Hii ni kutokana na Khaemba kutoa amri ya Waititu ambaye alikuwa anakumbwa na kesi ya ubadhirifu wa shilingi milioni 588 kuachiliwa kwa dhamana , licha ya kuwa katika kipindi cha mapumziko.

Khaemba baadaye alikubaliana na tume ya utumushi wa mahakama kumlipa mshahara wake wa kutoka 14/6/2019 hadi 31/12/2021.

“Hata kama niliamrishwa kurejea kazini na mahakama ya rufaa, nataka kujitenga rasmi na mwajiri wangu wa awali, ambaye ni, tume ya utumushi wa mahakama,” Khaemba alisema.

Aliishukuru mahakama ya Kenya kwa kumpa nafasi ya kuhudumu kama hakimu kwa zaidi ya miaka kumi.

“Kwa kweli ilikuwa ni nafasi ya kipekee kuwa hakimu katika viwango tofauti, ikifahamika kwamba nilijiunga na taasisi hiyo nikiwa na umri mdogo katika taaluma hii. Shukran nyingi kwa wenzangu wote ambao nilifanikiwa kufanya kazi nao,” aliandika Khaemba.

Aidha amesema kwamba hatua kubwa zaidi aliyoipiga ni kuhudumu kama katibu mkuu wa baraza la mahakimu na majaji nchini na baadaye  kuwa katibu mkuu wa mahakimu na majaji katika ukanda qwa Afrika Mashariki.

Khaemba amesema kwamba sasa anatazamia kuwahudumia wananchi katika viwango tofauti, kwa uwezo wa Mungu.

Hakimu huyo ametangaza azma yake  ya kuwania ubunge wa eneo la Kimilili kupitia chama cha Ford Kenya, nafasi hiyo ikishikiliwa na Didmus Barasa.