Barasa awachiliwa kwa dhamana ya 100,000 baada ya kukanusha mashtaka ya kushambulia mwanakandarasi

Barasa kwa upande wake alidai kuwa madai dhidi yake ni vita ya kisiasa ambayo inatekelezwa na mahasidi wake kwenye siasa.

Muhtasari

•Licha ya kurekodiwa akimzaba kofi mwanakandarasi huyo na video hiyo kuenezwa sana mitandaoni, Barasa alikanusha mashtaka ya kushambulia Masinde mbele ya mahakama.

•Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa naibu rais William Ruto alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Kimilili Jumatatu asubuhi akiwa nyumbani kwake maeneo ya Nasianda.

•Kesi hiyo itaendelea mnamo Septemba 27.

Didmus Barasa mahakamani siku ya Jumatatu
Didmus Barasa mahakamani siku ya Jumatatu
Image: JOHN NALIANYA

Habari na John Nalianya

Mnamo Jumatatu mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alifikishwa mahakamani kusomewa mashtaka  dhidi yake ya kusababisha majeraha  mabaya mwilini wa mwanakandarasi Stephen Wekesa Masinde.

Licha ya kurekodiwa akimzaba kofi mwanakandarasi huyo na video hiyo kuenezwa sana mitandaoni, Barasa alikanusha mashtaka ya kushambulia Masinde mbele ya mahakama.

Mwanasiasa huyo pamoja na wengine ambao hawakuwa pale mahakamani wanadaiwa kumsababishia Masinde majeraha mabaya mwilini mnamo Julai 30 walipokuwa katika shule ya msingi ya Lurare Baptist.

Mbunge huyo ambaye ni mwandani wa naibu rais William Ruto alikamatwa na maafisa wa polisi kutoka kituo cha Kimilili Jumatatu asubuhi akiwa nyumbani kwake maeneo ya Nasianda.

Hakimu Gladys Odhiambo alimuachilia mwanasiasa huyo kwa dhamana ya shilingi 100,000 baada yake kukanusha mashtaka.

Kesi hiyo itaendelea mnamo Septemba 27.

Wakili wa mlalamishi Brian Khaemba alipongeza polisi kwa kumkamata Barasa kwa upesi na kutaka haki kutendeka.

Khaemba alisema kuwa mahakamana ilikuwa imeagiza Barasa kutomtishia mlalamishi ambaye pia ni mwanamuziki tajika maeneo ya Magharibi mwa Kenya. 

"Tumewasilisha ombi la kutaka kesi hii kuhamishwa kutoka hapa Kimilili na kupelekwa kwa korti ingine nje ya eneo bunge hili. Hivo mteja wangu ambaye si mwenyeji wa hapa atakuwa salama na huru kuendelea na kesi" Wakili alisema. 

Barasa kwa upande wake alidai kuwa madai dhidi yake ni vita ya kisiasa ambayo inatekelezwa  na  mahasidi wake kwenye siasa.