Rais Kenyatta aamrisha kudumishwa kwa amani Marsabit

Muhtasari

• Rais Uhuru Kenyatta ametoa makataa ya wiki mbili kwa viongozi wa kaunti ya Marsabit kutafuta suluhu ya vita vya  jamii eneo hilo ambavyo vimedumu kwa muda sasa.

• Rais Kenyatta aliyazungumza hayo siku ya Jumanne alipoandaa mkutano na viongozi kutoka kaunti za Marsabit, Isiolo na Tana River.

Image: PSCU

Rais Uhuru Kenyatta ametoa makataa ya wiki mbili kwa viongozi wa kaunti ya Marsabit kutafuta suluhu ya vita vya  jamii eneo hilo ambavyo vimedumu kwa muda sasa.

Kenyatta alionya kwamba iwapo viongozi hao watakosa kupendekeza mikakati ya kumaliza vita hivyo, serikali kuu italazimika kupeleka vyombo vya usalama eneo hilo ambavyo vitakuwa chini ya amri kali na kutumia nguvu nyingi ili kutuliza hali katika kaunti hiyo.

“Rafiki zangu kutoka Marsabit, mnapaswa kuketi chini na kutafuta mbinu za kuleta amani miongoni mwenu. Lazima mtakubaliana na mlete suluhu kwa sababu tayari mnayo. Nitawatafuta baada ya wiki mbili, kama hamtaleta mapendekezo ya suluhu, basi mtakuwa mmeamua kwamba serikali kuu iingilie kati na mnajua hilo linamaanisha nini,” rais alisema.

Rais Kenyatta aliyazungumza hayo siku ya Jumanne alipoandaa mkutano na viongozi kutoka kaunti za Marsabit, Isiolo na Tana River.

Uhuru Kenyatta alisisitiza kuhusu haja ya viongozi kutoka kaunti ya Marsabit kubadilisha mfumo wao na kufanya kazi pamoja ili kudumisha amani badala ya kuchochea vurugu miongoni mwa wakazi.

“Amani ni jambo la muhimu sana ambalo lina faida nyingi. Dumisheni amani ili mnufaike kutoka kwa serikalim kuu. Badala ya kuchochea vurugu na mambo yasiyo na msingi, pambaneni kuboresha hali ya maisha ya watu wa Marsabit,” Kenyatta aliongezea.

Rais Uhuru Kenyatta aliwataka viongozi hao kuiga mfano wake na kinara wa chama cha ODM, Raila Odinga walivyoshikana mkono ili kuleta amani nchini.

Alimalizia kwa kuwarai viongozi wote kutokubali siasa kuleta tofauti miongoni mwao badala yake kufanya kazi pamoja ili kuunganisha taifa kwa ujumla.