Herman Manyora aonya dhidi ya tofauti za Kenyatta na Ruto

Muhtasari

• Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Herman Manyora amewaomba rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kukoma kutupiana maneno makali wanapokuwa katika majukwaa ya kampeni.

• Manyora amewarai wakenya kufanya maamuzi ya kibusara itakapowadia tarehe 9/8/2022 ili kuhakikisha wanamchagua kiongozi ambaye atapigania masilahi yao.

Herman Manyora
Herman Manyora
Image: Instagram KWA HISANI

Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa, Herman Manyora amewaomba rais Uhuru Kenyatta na naibu wake William Ruto kukoma kutupiana maneno makali wanapokuwa katika majukwaa ya kampeni.

 Akizungumza kupitia video aliyopakia katika akaunti yake ya YouTube, Manyora amesema kwamba wawili hao wanapaswa kuwaheshimu wananchi wanaowaongoza na kukoma kuonyesha chuki zao waziwazi kwa umma na badala yake kuangazia maendeleo kwa wananchi.

Manyora amemsihi naibu rais William Ruto kumheshimu rais Kenyatta pamoja na ofisi yake na kusubiri wakati wake ambapo atafanikiwa kuchaguliwa kuwa kiongozi wa taifa.

Kulingana na mchanganuzi huyo, uhusiano wa rais na naibu wake ulisambaratika katika awamu yao ya kwanza walipoingia serikalini kupitia chama cha Jubilee.

Aidha, ametaja kwamba rais Kenyatta amefanikiwa kuleta maendeleo kadhaa chini ya uongozi wake na kuonya dhidi ya viongozi wanaomuunga mkono naibu rais William Ruto kuepuka cheche zitakazozua ghasia za baada ya uchaguzi.

Manyora amewarai wakenya kufanya maamuzi ya kibusara itakapowadia tarehe 9/8/2022 ili kuhakikisha wanamchagua kiongozi ambaye atapigania masilahi yao.