Kundi la fisi lashambulia na kuua mwanaume Juja

Muhtasari

•Robert Mwangi, 31, alishambuliwa na zaidi ya fisi wanane wakati kijiji kikiwa tulivu kwani watu wengi walikuwa ndani ya nyumba zao.

hyena
hyena
Image: HISANI

Jamaa mmoja alipoteza maisha yake usiku wa Alhamisi baada ya kushambuliwa na kikundi cha fisi katika kijiji cha Athi, eneo la Juja.

Robert Mwangi, 31, anaripotiwa kuvamiwa na zaidi ya fisi wanane wakati  kijiji kikiwa tulivu kwani watu wengi walikuwa ndani ya nyumba zao.

Inaripotiwa kuwa marehemu alisikika akipiga nduru katika juhudi za kuomba usaidizi ila wanakijiji hawakufanikiwa kumuokoa kwa wakati.

Mabaki ya marehemu yalipatikana yakiwa yamelala chini na kupelekwa katika mochari ya General Kago.

Haya yanajiri miezi miwili baada ya wanyama hao kuhangaisha wakazi wa baadhi ya maeneo ya Kiambu na kuua takriban wawili.

Mwanaume mmoja alipatika akiwa ameuliwa na wanyama hao katika kijiji cha Kang'oki mwishoni mwa mwezi Desemba na mwingine akashambuliwa katika eneo la Kamuthi siku moja baadae.

Maafisa wa DCI walihimza wakazi wa Thika na Juja kuwa makini na waangalifu zaidi huku wakiahidi kuwawinda fisi ambao walikuwa wanatembea pale na kuwarejesha kwenye mbuga la wanyama.