Jamaa ashambuliwa na kundi la fisi 20 hadi kifo Juja

Muhtasari

•Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 29 alikuwa ameandamana na mwenzake wakirejea nyumbani kutoka kwa machimbo ya Komu wanakotafutia riziki wakati kundi la fisi wapatao 20 walipowavamia.

hyena
hyena
Image: HISANI

Jamaa mmoja anaripotiwa kushambuliwa na kundi la fisi hadi kifo  mwendo wa saa kumi na moja alfajiri ya Jumatatu katika eneo la Kamuthi, kaunti ndogo ya Juja.

Jamaa huyo mwenye umri wa miaka 29 alikuwa ameandamana na mwenzake wakirejea nyumbani kutoka kwa machimbo ya Komu wanakotafutia riziki wakati kundi la fisi wapatao 20 walipowavamia.

Marehemu alipoteza maisha yake papo hapo huko mwenzake akinusurika kifo kwa tundu la sindano baada ya kutimuka mbio.

Kufuatia shambulio hilo la fisi wanaosemekana kuponyoka kutoka kwa mbuga la wanyama na wanaoendelea kusababisha madhara, wakazi wa eneo la Witeithie wamehimizwa kuwa waangalifu wanapotembea.

Kitengo cha upelelezi wa Jinai (DCI) hata hivyo kimewahakikishia wakazi kuwa maafisa husika wanaendelea kushughulikia suala hilo.

"Tunazidi kuwa ange kuhakikisha usalama katika msimu huu wa sherehe huku kauli mbiu yetu ikiwa bado ni Kujitolea, Kujali na Uadilifu!" DCI wamesema.