Kalonzo atoboa siri za makubaliano yake na Odinga ndani ya NASA

Muhtasari

• Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka kwa mara ya kwanza ameweka wazi mambo mengi ya siri kuhusu makubaliano yake na kinara wa ODM Raila Odinga walipokuwa chini ya muungano wa NASA.

• Mkataba huo wa makubaliano kati yao ulitiwa sahihi mnamo aterehe 30/4/2017.

HE Kalonzo Musyoka akihutubia wanahabari katika Kituo cha Amri, Karen mnamo Jumanne Machi 1 wakati wa mkutano na wanahabari kuhusu mikataba ya NASA kati ya Raila Odinga na Kalonzo wakati wa uchaguzi wa 2017.
Image: Wilfred Nyangaresi

Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka kwa mara ya kwanza ameweka wazi mambo mengi ya siri kuhusu makubaliano yake na kinara wa ODM Raila Odinga walipokuwa chini ya muungano wa NASA.

Katika makubaliano hayo yaliyowekwa wazi siku ya Jumanne,viongozi hao walikubaliana kwamba Raila Odinga angepeperusha bendera ya NASA huku Kalonzo Musyoka akichukua nafasi ya mgombea mwenza.

Mkataba huo wa makubaliano kati yao ulitiwa sahihi mnamo aterehe 30/4/2017.

“Raila amekubaliana katika mkataba huu kwamba atahudumu kama rais kwa awamu moja[miaka mitano] halafu baadaye kumzindua Kalonzo hadharani kama mgombeaji wa urais katika mwaka wa 2022,” mkataba huo ulisoma.

Baada ya miaka mitatu kama rais, Odinga alihitajika kugawa asilimia kubwa ya majukumu makubwa katika serikali kwa Musyoka huku yeye akizingatia majukumu ya kimataifa.

“Wawili hao walikubaliana kwamba kipengele cha Kalonzo kupewa asilimia kubwa ya majukumu ya serikali kuu baada ya miaka mitatu, hakingewekwa hadharani,” makubaliano hayo yalisema.

Vilevile, wawili hao waliafikiana kugawanya fedha za kampeni katika kipindi cha uchaguzi wa 2017.

“Walikubaliana kuhutubia umma kote nchini hasahsa eneo la Nyanza, Magharibi mwa Kenya, bonde la ufa na Pwani ya Kenya ili kuwaelezea wananchi kuhusu muungano wao,” makubaliano hayo yaliendelea kueleza.

Musyoka alisema kwamba wakili Makau Mutua alishuhudia wawili hao wakitia sahihi katika makubaliano hayo ila alidinda kuita mkutano kati yake na Raila Odinga ili kujadiliana kuhusu makubaliano kuhusu muungano wao wa 2017.

Huku Kalonzo kwamba amejaribu kumtafuta Makau Mutua bila mafanikio, ameshikilia kwamba Raila Odinga anapaswa kutekeleza makubaliano yao ili atajwe kama shujaa wa kidemokrasia.