Bajeti ya mwisho ya rais Uhuru ni haramu na kinyume cha katiba- Duale

Muhtasari

•Duale alisema waziri wa Hazina, Ukur Yatani alikiuka taratibu za kuandaa bajeti ambazo zilifaa kufanywa na Bunge la Kitaifa. 

• Duale alibainisha kuwa Waziri wa Hazina hajapata kibali cha Bunge la Kitaifa katika matangazo fulani ambayo atatarajiwa  kutoa leo.

Mbunge wa Garissa Aden Duale
Mbunge wa Garissa Aden Duale
Image: MAKTABA

Aliyekuwa kiongozi wa wengi bungeni Aden Duale sasa anasema kuwa zoezi la usomaji wa bajeti ya 2022/2023 katika Bunge la Kitaifa ni kinyume cha sheria na ni ukiukaji wa katiba. 

Akizungumza katika majengo ya bunge siku ya Alhamisi, Duale alisema waziri wa Hazina, Ukur Yatani alikiuka taratibu za kuandaa bajeti ambazo zilifaa kufanywa na Bunge la Kitaifa. 

Alimlaumu Yatani kwa kunyakua kazi ya Bunge katika uundaji wa bajeti, hatua ambayo anasema ni kinyume cha sheria na ni ukiukaji wa katiba.

 “Anachofanya waziri ni kinyume cha sheria kwa sababu jukumu la mchakato wa kutengeneza bajeti ni la Bunge,” alisema.

“Kwa mara ya kwanza, waziri amenyakua jukumu hilo. Bunge limepewa mamlaka ya kutengeneza bajeti.”

 Duale alibainisha kuwa Waziri wa Hazina hajapata kibali cha Bunge la Kitaifa katika matangazo fulani ambayo atatarajiwa  kutoa leo. (Alhamisi.) 

 "Hajaleta makadirio ya mapato na matumizi bungeni, anatangaza matamko bila kibali cha Bunge," alisema.

"Nyumba inapoteza uwezo wake na kutoka mahali ninapokaa sitasikiliza bajeti hii."