Serikali kuendelea kuwianisha mafunzo ya kijeshi kuambatana na mahitaji ya usalama

Muhtasari

•Rais alisema uwezo wa vikosi vya kijeshi nchini hauzingatii tu vifaa vya kisasa bali pia utaalamu wa maafisa wake.

 

•Alisema ununuzi wa ndege za kisasa na ubunifu wa kituo hicho cha mafunzo kutasaidia Jeshi la humu nchini na mashirika mengine ya serikali kutimiza majukumu mbali mbali katika shughuli za angani.

Image: STATEHOUSE TWITTER

Rais Uhuru Kenyatta amekariri kujitolea kwa Serikali kuendelea kuzindua mipango inayonuiwa kuwianisha mafunzo ya kijeshi nchini kuhakikisha yanalingana na mahitaji ya kiusalama na kiraia.

Kiongozi wa nchi alisema uwezo wa vikosi vya kijeshi nchini hauzingatii tu vifaa vya kisasa bali pia utaalamu wa maafisa wake.

Rais ambaye ni Amiri-Jeshi-Mkuu wa Vikosi vya Kijeshi nchini alisema haya siku ya Alhamisi katika kambi ya Laikipia ya Jeshi la Wanahewa mjini Nanyuki ambako alizindua Kituo cha Ubora wa Mafunzo cha jeshi la humu nchini (KDF).

Kituo hicho cha kisasa cha kutoa mafunzo ya marubani na maafisa wa kiufundi kimebuniwa na Jeshi la humu nchini kama mojawapo wa harakati za kuimarisha uwezo wa ulinzi na usalama wa jeshi.

“Kituo hiki kinadhihirisha kwamba hatuzingatii tu vifaa. Jeshi lolote la kisasa na linalostawi sharti lizingatie ustadi wa mafunzo ambao ni muhimu katika kuimarisha shughuli za kutimiza majukumu yao,” kasema Rais Kenyatta.

Image: STATEHOUSE TWITTER

Alisema ununuzi wa ndege za kisasa na ubunifu wa kituo hicho cha mafunzo kutasaidia Jeshi la humu nchini na mashirika mengine ya serikali kutimiza majukumu mbali mbali katika shughuli za angani.

“Natoa changamoto kwa kituo hiki kujumuisha Jumuiya ya Afrika Mashariki na maeneo mengine katika kutoa mafunzo ya utaalamu wa ndege. Hatua hii haipaswi kuzingatia tu washikadau wa sekta za usalama bali pia kusambaza huduma zake katika mashirika ya raia kama vile shirika la ndege la Kenya Airways na mashirika mengine ya ndege ambayo yanahitaji maafisa wenye utaalamu bora,” kasema Rais.

Kiongozi wa nchi alisema Jeshi la humu nchini limepokea mitambo mipya ya taratibu za safari za ndege na akatangaza mipango ya kununua  vifaa vipya vya kisasa vya kukagua anga ya baharini kuliwezesha jeshi kushughulikia kwa makini vitisho vinavyoibuka vya usalama wa kitaifa.

“Juhudi hizi zitahakikisha kwamba vikosi vyetu vya usalama vina vifaa vya kutosha kutimiza majukumu yao ya kikatiba ya kuhakikisha usalama wa kitaifa. Vile vile, uwezo huu ulioimarishwa utasambaza uwezo wa Kenya kuchangia jitihada za kukabiliana na majanga nchini na katika  eneo hili,” kasema Rais.

Kwa mara nyingine, Rais Kenyatta alikariri umuhimu wa usalama kwa ajenda ya mabadiliko ya ustawi wa kijamii na kiuchumi nchini .

“Hakika, usalama ni msingi wa kujitawala kwetu, uhuru wetu, demokrasia yetu  na mdhamini wa maisha yetu. Na kwa sababu hiyo, tuna deni kubwa la shukrani kwa  jeshi letu la usalama.

“Hivyo basi, katika miaka tisa ambayo nimebahatika kuhudumu kama Amiri Jeshi wenu, tumetekeleza mabadiliko ya sekta ya usalama ambayo yameimarisha uwezo, uthabiti na maslahi bora ya jeshi letu,” kasema Rais.

Image: STATEHOUSE

“Tuna fahari kuu kwa wote wanaohudumu katika mstari wa mbele katika majukumu na shughuli mbali mbali hasa mashujaa wetu waliojeruhiwa ambao wana makovu yanayoonekana na yasiyoonekana ya huduma kwa Jamhuri,” Rais kawapongeza wanajeshi wa Kenya.

Katika kutambua mchango mkubwa na kujitolea kwa jeshi la ulinzi nchini, Rais  alihimiza Bunge kuharakisha kupitisha  Mswaada wa Wanajeshi waliostaafu.

Katika hotuba yake, Waziri wa Ulinzi Eugene Wamalwa alisema KDF ilikuwa katika msitari wa mbele wa teknolojia mpya akiongeza kwamba wizara yake imeridhika na ustawi uliotekelezwa kuifanya jeshi kuwa la kisasa.

Bw. Wamalwa alisema Kituo cha Mafunzo cha Ubora cha Wataalamu wa Ndege cha Jeshi la Ulinzi nchini kimechipua teknolojia mpya na kuimarisha mafunzo ya marubani wa kijeshi na wataalamu wengine wa kiufundi.

Mkuu wa Majeshi Generali Robert Kibochi alimshukuru Rais  Kenyatta kutokana na uekezaji wa serikali unaoendelea katika jeshi akisema kituo kilichozinduliwa kitasaidia kupunguza gharama ya kutoa mafunzo  kwa wataalamu wa ndege.

Mawaziri Mutahi Kagwe (Afya), Peter Munya (Kilimo) na Gavana Ndiritu Muriithi wa Laikipia walikuwa baadhi ya maafisa wakuu serikalini na wa kijeshi waliohudhuria hafla hiyo.