5 wafariki, 12 hawajulikani walipo baada ya washambuliaji kuvamia maafisa wa serikali Marsabit

Muhtasari

•Wahasiriwa walikuwa wakisaka ng'ombe walioibwa katika eneo la Awaye walipovamiwa na washambuliaji hao.

•Koo zimekuwa zikishambuliana mara kwa mara na kuwaacha wengi wakiwa wamepoteza maisha na wengine kuyahama makazi yao.

crime scene
crime scene

Watu watano wakiwemo Chifu na Naibu Chifu waliuawa Alhamisi na watu wenye silaha katika Kaunti ya Marsabit.

Watu wengine kumi na wawili hawajulikani waliko kufuatia tukio hilo.

Polisi walisema MCA wa wadi ya Loglogo, Bernard Leakono ni miongoni mwa waliotoweka.

Chifu Mwandamizi wa Logogo Kennedy Kongoman, Chifu Msaidizi wa Lokileleng'i Keena Moga na wahasiriwa wengine watatu walikuwa wakisaka ng'ombe walioibwa katika eneo la Awaye walipovamiwa na washambuliaji hao.

Miili yao ilipatikana ndani ya magari mawili ambayo yalikuwa yametelekezwa barabarani baada ya kupigwa risasi.

Kulingana na Kamishna wa Kaunti ya Marsabit Paul Rotich, Washambuliaji hao walitoroka mara baada ya uvamizi huo. Haijabainika iwapo waliwabeba wakazi waliotoweka.

Rotich alisema watu 12 waliotoweka pia walikuwa sehemu ya timu iliyokuwa ikiwasaka mifugo hao.

"Vikosi vinaungana huko kuwafuata washambuliaji na kuwatafuta watu waliopotea," alisema.

Dalili za shambulio hilo zimekuwepo huku koo zikishambuliana mara kwa mara na kuwaacha wengi wakiwa wamepoteza maisha na wengine kuyahama makazi yao.

Wenyeji walisema polisi walikosa helikopta ya kusaidia kufika katika eneo la tukio na kuwafuata washambuliaji.

Chopa za polisi zimezuiwa na zile za mashirika mengine zinatumika kwingine nanhivyo  kuviweka vyombo vya usalama kwenye hatari zaidi.

Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang'i alikuwa ameonya kuwa serikali itaanzisha operesheni kali katika eneo hilo ili kudhibiti visa vya uvamizi. 

Alisema serikali imedhamiria kutafuta suluhu la mzozo huo katika baadhi ya maeneo ya kaunti za Marsabit, Laikipia, Samburu na Baringo.

Makumi ya watu wameuawa katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita katika kile kinachoonekana kama mchezo wa kisiasa wa kudhibiti rasilimali za ndani.

Mnamo Februari 22, Rais Uhuru Kenyatta aliwapa viongozi wa Marsabit wiki mbili kuangazia suluhu la kudumu la mizozo ya jamii ambayo imedumaza kaunti hiyo.

Hata hivyo, hali bado haijatulia.