Washukiwa wawili wa uhalifu wa kifo watoroka kutoka gereza la Kirinyaga

OCPD wa Kirinyaga Central aliwataja wafungwa tu kuwa ni wanaume wa umri wa makamo.

Muhtasari

•Wafungwa hao wanasemekana kutoroka saa saa kumi kasorobo asubuhi kwa kuruka nje kupitia ukuta wa mzunguko wa gereza hilo.

•OCPD aliwataja washukiwa hao kuwa ni hatari kwa usalama wa kaunti hiyo na hivyo amewataka wananchi kuwa waangalifu.

Ubao wa ishara wa gereza la GK Kerugoya.
Ubao wa ishara wa gereza la GK Kerugoya.
Image: WANGECHI WANG'ONDU

Polisi katika kaunti ya Kirinyaga wanawasaka wafungwa wawili waliotoroka katika gereza la G.K Kerugoya alfajiri ya Jumatatu.

Wafungwa hao wanaokabiliwa na mashtaka makubwa wanasemekana kutoroka saa saa kumi kasorobo asubuhi kwa kuruka nje kupitia ukuta wa mzunguko wa gereza hilo.

OCPD wa Kirinyaga ya kati John Torori aliambia wanahabari kuwa wawili hao walikuwa katika kundi la wafungwa watatu ambao awali walifanikiwa kutoroka hata hivyo mmoja alikamatwa baada ya muda mfupi kupitia usaidizi wa wananchi.

Mkuu huyo wa polisi aliwataja washukiwa hao kuwa ni hatari kwa usalama wa kaunti hiyo na hivyo amewataka wananchi kuwa waangalifu na kutoa taarifa kwa watu wanaotilia shaka katika kituo cha polisi kilicho karibu.

Ingawa alisita kutaja majina yao kutokana na unyeti na uzito wa mashtaka yao, bosi huyo wa polisi aliwataja tu kuwa ni wanaume wa umri wa makamo.

Aliongeza kuwa bado hawajajua njia waliyopitia washukiwa wakati wa kutoroka. Hata hivyo, alibainisha kuwa mmoja wa waliotoroka alipata jeraha la risasi kutoka kwa maafisa ambao walikuwa wakifuatilia harakati zao.

"Tulipokea taarifa kutoka kwa kituo cha gereza kuhusu kutoroka kwa wafungwa waliokuwa wamewekwa chini ya ulinzi. Tulifanikiwa kuwahamasisha maafisa wetu kuwafuatilia na kwa usaidizi wa wananchi, tulifanikiwa kumkamata mhalifu mmoja."

"Hata hivyo bado hatujajua wawili walitorokea wapi. Polisi wako katika hali ya tahadhari na operesheni kali inafanywa ili kuwakamata." Alisema.