Kenya kuanza kesi dhidi ya maafisa wa 'kikosi cha polisi wauaji'

Kitengo hicho kilivunjwa baada ya rais kupokea ripoti ya polisi kuhusu kutoweka kwa raia wawili wa India.

Muhtasari

•Maafisa wa Kitengo cha Huduma Maalum kilichovunjwa sasa wanakabiliwa na mashtaka mengi yakiwemo mauaji, matumizi mabaya ya ofisi na kula njama ya kutenda uhalifu.

•Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa na ya ndani sasa unaitaka serikali kuwafungulia mashitaka maafisa hao, na kuwalipa fidia waathiriwa wa unyanyasaji wa polisi.

Image: BBC

Polisi wanne wa Kenya wanaodaiwa kuhusika na msururu wa mauaji, utekaji nyara na mateso kote nchini wanatarajiwa kufikishwa mahakamani Jumatatu katika mji mkuu, Nairobi.

Walikuwa sehemu ya kikosi maalum ambacho kilivunjwa na Rais William Ruto kwa madai ya kutekeleza mauaji ya kiholela na kutoweka kwa washukiwa kwa miaka kadhaa.

Miongoni mwa wanaodaiwa kuwa wahasiriwa wa hivi punde ni raia wawili wa India waliotoweka mwezi Julai na ambao mabaki yao yaligunduliwa wiki iliyopita katika msitu mmoja katikati mwa Kenya.

Wanachama wa Kitengo cha Huduma Maalum kilichovunjwa sasa wanakabiliwa na mashtaka mengi yakiwemo mauaji, matumizi mabaya ya ofisi na kula njama ya kutenda uhalifu.

Kitengo hicho kilivunjwa baada ya rais kupokea ripoti ya polisi kuhusu kutoweka kwa raia hao wawili wa India.

Zulfiqar Ahmad Khan na Mohamed Zaid Sami Kidwai walikuwa nchini Kenya kusaidia kampeni za uchaguzi za Bw Ruto, lakini walitoweka pamoja na dereva wao wa eneo hilo Nicodemus Mwania mara baada ya kuchukuliwa na polisi jijini Nairobi.

Mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema uchunguzi wao huru umehusisha kikosi hicho na vitengo vingine vya polisi na vifo vya zaidi ya watu 600 katika kipindi cha miaka minne iliyopita.

Baadhi ya miili hiyo ilipatikana baadaye katika mito magharibi na kaskazini mwa Kenya.

Muungano wa mashirika yasiyo ya kiserikali ya kimataifa na ya ndani sasa unaitaka serikali kuwafungulia mashitaka maafisa hao, na kuwalipa fidia waathiriwa wa unyanyasaji wa polisi.