Nimemalizana na wewe, Oparanya amwambia Raila

Oparanya, ambaye ni naibu wa Raila katika ODM, alisema ataangazia harakati za kuleta umoja wa jamii ya Luyha.

Muhtasari

• Wabunge wa jamii ya Luhya siku ya Jumanne walimshutumu Raila kwa usaliti katika ugavi wa nafasi za wachache Bungeni.

• Wabunge walidai kuwa Raila alitenga jamii hiyo katika nafasi kwenye Tume ya Huduma za Bunge pamoja na nyadhifa za uongozi wa wachache bungeni.

 

Gavana Wycliffe Oparanya
Gavana Wycliffe Oparanya
Image: THE STAR

Aliyekuwa gavana wa Kakamega Wycliffe Oparanya amesema hana biashara tena na kinara wa upinzani Raila Odinga.

Msimamo wa hivi punde wa Oparanya huenda ukawa pigo  kwa siasa za Raila ambaye alikuwa akimtegemea sana Oparanya kupata uungwaji mkono kutoka jamii ya Luyha.

Oparanya, ambaye ni naibu wa Raila katika chama cha ODM, alisema kuanzia sasa ataangazia harakati za kuleta umoja wa jamii ya Luyha.

Baada ya kumuunga mkono Raila mara tano bila mafanikio, Oparanya alisema, ni wakati wa jamii ya Luyha kujipanga kisiasa kabla ya uchaguzi wa 2027.

"Ninajitolea kuanzia sasa kuongoza harakati za umoja wa watu wetu. Nimemalizana na Raila na hata akinisema mabaya, Mungu akemee mbali, anajua, hatasamehewa,” Oparanya alisema.

Oparanya, ambaye aliongoza kampeni za urais za Azimio Magharibi mwa Kenya, alimshutumu Raila kwa usaliti wa kisiasa.

Hata hivyo, hakusema iwapo ataondoka ODM au la.

Alisema uungwaji mkono na ufuasi ambao ambao Raila amepata kutoka Magharibi kwa miongo kadhaa haujazingatiwa katika ugavi wa nafasi za kisiasa.

Kwa mfano, Oparanya alishangaa kwa nini jamii ya Luyha haikupewa hata nafasi moja katika Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

"Matokeo ya kura hiyo ni kwamba makabila mengine yote makubwa isipokuwa lakini Waluhya walipata mbunge kwa EALA," alisema Jumanne wakati wa mazishi katika kijiji cha Ichinga, Mumias Mashariki.

Alikuwa amehudhuria mazishi ya MCA maalum Phaustine Welimo.

Gavana huyo alikuwa akimpigia debe aliyekuwa Mbunge wa Shinyalu Justus Kizito katika uchaguzi wa EALA lakini mwanasiasa huyo akashindwa Bungeni.

  “Nilikuwa nikishinikiza Kizito Justus aende EALA lakini wabunge walikuwa wakinung’unika kwamba Kizito hana pesa. Nilishangaa kwamba wabunge lazima pia wahongwe ili wapige kura,” alisema.

Matamshi ya Oparanya yanaonekana kuiana na yale ya baadhi ya wabunge wa jamii ya Luhya siku ya Jumanne waliomshutumu Raila kwa usaliti katika ugavi wa nafasi za wachache Bungeni.

Wabunge walidai kuwa Raila alitenga jamii hiyo katika nafasi kwenye Tume ya Huduma za Bunge pamoja na nyadhifa za uongozi wa wachache bungeni.

 

IMETAFSIRIWA NA DAVIS OJIAMBO