Seneti yapendekeza kamati ya watu 11 kumchunguza gavana Kawira

Kamati ya Seneti ya Biashara iliomba Bunge kuidhinisha majina 11 ambayo imependekeza kuketi kwenye jopo.

Muhtasari

•Kamati ya Biashara ya Seneti iliomba Bunge kuidhinisha majina 11 ambayo imependekeza kuketi kwenye jopo hilo.

•Miongoni mwa maseneta ambao majina yao yametajwa kuketi katika jopo hilo ni kinara wa wengi Boni Khalwale , Jackson Mandago , Karungo Thangwa, na Ali Roba.

GAVANA WA MERU KAWIRA MWANGAZA
Image: KAWIRA MWANGAZA/FACEBOOK

Uongozi wa Seneti umependekeza kuundwa kwa kamati maalum ya kuchunguza mashtaka dhidi ya gavana wa Meru aliyezingirwa Kawira Mwangaza.

Katika kikao kilichofanyika Jumanne asubuhi, Kamati ya Biashara ya Seneti iliomba Bunge kuidhinisha majina 11 ambayo imependekeza kuketi kwenye jopo hilo.

Kiongozi wa Wengi katika Seneti Aaron Cheruiyot ameratibiwa kutoa hoja wakati wa kikao maalum ya kuundwa kwa kamati hiyo Jumanne alasiri.

“Seneti inaazimia kuunda kamati maalum kuchunguza mapendekezo ya kuondolewa afisini kwa Gavana wa Kaunti ya Meru,” hoja hiyo inasomeka kwa sehemu.

Miongoni mwa maseneta ambao majina yao yametajwa kuketi katika jopo hilo ni kinara wa wengi Boni Khalwale (Kakamega), Jackson Mandago (Uasin Gishu), Karungo Thangwa (Kiambu) na Ali Roba (Mandera).

Maseneta wengine ni Esther Okenyuri (wa kuteuliwa), Peris Tobiko (wa kuteuliwa), Eddy Oketch (Migori), Joseph Kamau (Lamu), Edwin Sifuna (Nairobi), Agnes Kavindu (Machakos) na Johnes Mwaruma (Taita Taveta).

Kifungu cha 33 cha Sheria ya Serikali za Kaunti kinasema kwamba Seneti inaweza kutekeleza kubanduliwa kwa gavana kupitia kamati maalum au kikao.