La hasha! rais Ruto asema hataruhusu ushoga Kenya, akosoa mahakama ya upeo

Hiyo haiwezekani katika taifa letu. Itafanyika kwingine lakini haitafanyika Kenya".

Muhtasari

• Rais alisema vigezo hivi haviwezi kuruhusu kamwe mtu yeyote kushiriki katika mapenzi na mtu wa jinsia yake.

Rais William Ruto akitoa marufuku kwa wafugaji kutumia bunduki.
Rais William Ruto akitoa marufuku kwa wafugaji kutumia bunduki.
Image: Facebook

Rais William Ruto amekemea vikali uamuzi wa mahakama ya upeo kuruhusu wanachama wa LGBTQ kusajili muungano wao.

Rais Ruto siku ya Alhamisi alitangaza wazi msimamo wake kuhusu shughuli za wapenzi wa jinsia moja nchini Kenya LGBTQ akisema kuwa ingawa anaheshimu mahakama kama idara iliyotwikwa jukumu la kufafanua sheria,kuna vipengele vinavyohusishwa na jamii ya Kenya ikiwemo mila,desturi na dini ambavyo vinafaa kuzingatiwa kila mara uamuzi unatolewa na mahakama.

 

Rais alisema vigezo hivi haviwezi kuruhusu kamwe mtu yeyote kushiriki katika mapenzi na mtu wa jinsia yake.

Kiongozi wa taifa alikariri kuwa kulingana na mila na desturi za wakenya,haiwezekani kutetea shughuli za ushoga nchini. Alisema jambo hilo haliwezi kufanyika katika taifa la Kenya.

Rais aliwahakikishia Wakenya kutokuwa na shaka kuhusu jambo hilo kwani hawezi kuruhusu humu nchini. 

Ruto vile vile aliwaomba viongozi wa kidini kutilia mkazo ushauri kwa vijana, watoto,wanafunzi na wananchi kwa jumla kukuza mila na destruri bora ili wasipoteze asili zao kwa manufaa ya kizazi kijacho.

 

"Hata kama tunaheshimu korti lakini desturi na mila na dini haziwezi kuruhusu mwanamume amuoe mwanamume mwenzake au mwanamke amuoe mwanamke mwezake. Hiyo haiwezekani katika taifa letu. Itafanyika kwingine lakini haitafanyika Kenya", Ruto alikariri.

Msimamo wa rais umejiri baada ya viongozi wa kidini  kumtaka azungumzie jambo hilo.

Uamuzi wa mahakama ya upeo kuruhusu wanachama wa LGBTQ kusajili muungano wao umezua mjadala mkali nchini huku viongozi mbali mbali katika jamii wakikosoa uamuzi huo na kutaka serikali kutangaza msimamo wake na kukinga vijana wa taifa dhidi ya kuiga hulka potovu za ughaibuni.

MHARIRI: DAVIS OJIAMBO.