LGBTQ wanataka kueneza ajenda zao shuleni kwa njia ya kutoa ushauri nasaha - Daddy Owen

Msanii huyo alisema jamii ya LGBTQ inapanga mikakati ya kuwashawishi watoto shuleni kujiunga nao.

Muhtasari

• Owen alisema amepokezwa vitisho vya kunyimwa visa kwenda Marekani na pia kufungiwa mitandao ya kijamii kutokana na pingamizi zake dhidi ya LGBTQ.

Daddy Owen aapa kupinga LGBTQ Kenya hadi mwisho.
Daddy Owen aapa kupinga LGBTQ Kenya hadi mwisho.
Image: Instagram

Ijumaa wiki jana, jopo la majaji wa mahakama ya upeo lilipitisha uamuzi kuhalalisha ujumuikaji wa makundi ya wapenzi wa jinsia moja, uamuzi ambao umetajwa na wengi kuwa wa “kukanganya”

Kwa Zaidi ya siku tatu sasa, makundi mbalimbali haswa madhehebu mbalimbali wamejitokeza hadharani kulaani uamuzi huo wa mahakama wakisema kuwa majaji hao wanajaribu kuhalalisha dhambi.

Mwanamuziki wa injili wa muda mrefu Daddy Owen pia amejitosa katika mjadala huo na kuibua mazito kuhusu njama ya makundi ya LGBTQ kueneza ajenda zao nchini.

Owen ambaye alikuwa anazungumza kwenye mahojiano na kituo kimoja cha redio, alifichua kwamba ameshatumiwa wanyara wa siri jinsi LGBTQ wanapanga kusukuma ajenda zao katika shule wakilenga kuwashawishi wanafunzi kujiunga na jamii ya wapenzi wa jinsia moja.

Alisema kwamba katika waraka huo wa kinyemela, wanaorodhesha jinsi watafanikisha hilo kwa kuzuru shule wakijifanya wanatoa ushari nasaha kwa watoto kuhusu afya ya akili lakini ndani mwake wakihubiri injili ya LGBTQ.

“Mimi kama mzazi cha kwanza siwezi kubali. Cha pili mimi ni mwanamuziki wa injil, siwezi kubali. Sasa hivi hii si kwa Sanaa ya injili tu, imeingia kwa nchi nzima. Nimetumiwa waraka wa siri sana, njama ni kuingia kwenye shule kusema ni mambo ya ushauri nasaha na mafunzo kuhusu afya ya akili. Na hiyo ajenda tumeiona kwa umbali, haitakubalik!” alifoka Owen kwa ghadhabu.

Msanii huyo alisema anajua fika yale ambayo yatamuandama kutokana na msimamo wake mkali dhiti ya LGBTQ ikiwemo kufungiwa mitandao yake ya kijamii na kunyimwa visa ya kwenda Marekani.

Lakini alisimama kidete na kusema kwamba haogopi chochote na wala hakati kwenda Marekani.

“Sitaki kwenda Amerika mimi, wanasema wananifungia Instagram, wacha wafunge, tulihubiri injili miaka 20 bila mitandao ya kijamii. Na ikibidi tutaenda hadi bungeni kupinga hili,” Owen alisema.