Spika Wetang'ula atoa wito kwa umma na mahakama kulinda maadili ya taifa dhidi ya LGBTQ

Tamko lake linakuja siku tatu baada ya jopo la mahakama ya upeo kupitisha uamuzi kuwa LLGBTQ wana haki ya kujumuika.

Muhtasari

• Baada ya uamuzi huo, mjadala wa LGBTQ umewagawanya Wakenya kwa makundi tofauti.

SPIKA MOSES WETANGULA
Image: HISANI

Spika wa bunge la kitaifa Moses Wetang’ula amekuwa mtu wa hivi punde kujitosa katika mjadala unaozidi kuenea kuhusu hatua ya mahakama ya upeo kuhalallisha ujumuikaji wa makundi ya wapenzi wa jinsia moja – LGBTQ.

Wetang’ula kupitia ukurasa wake wa twitter alisema kwamba uamuzi huo wa mahakama ya upeo unaweza ukasababisha mgawanyiko mbaya sana nchini na kuleta madhara ambayo hayajawahi kufikirika.

Vile vile, spika Wetang’ula alisisitiza Kenya ni nchi ya Kidini mno yenye watu ambao wanafuata miongozo ya vitabu vitakatifu vinavyoorodhesha taratibu kuhusu uumbaji wa Mungu.

“Kenya ni nchi ya kidini sana. Kila mtu binafsi na/au taasisi ya Umma, ikijumuisha mahakama, ina wajibu wa kusimamia, kutetea na kulinda maadili ya umma!! Uamuzi wa mahakama ya upeo unaweza kusababisha matokeo yasiyotarajiwa na yasiyofaa,” Wetang’ula alionya.

Tamko hili linakuja siku tatu baada ya jopo la majaji wa mahakama hiyo ya juu Zaidi nchini kupitisha uamuzi kuwa makundi ya LGBTQ yana haki na uhuru wa kujumuika.

Makanisa mbali mbali yakiwemo kanisa katoliki kupitia kwa askofu mkuu wa dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria, CITAM, SDA na mengine yamejitokeza wazi na kulaani uamuzi huo huku wakijitenga na vitendo vyovyote vya LGBTQ humu nchini.

Wiki mbili zilizopita, kanisa la Kiangilikana nchini Uingereza lilisema lingeandaa kura kwa maaskofu wake kubaini iwapo wangepitisha sheria ya kutoa “baraak za mungu” kwa ndoa za wapenzi wa jinsia moja.