Raila atangaza maandamano ya kitaifa na kuzindua Vuguvugu la MDD

Alisema kuwa alimpa muda Rais Ruto ila hakutii.

Muhtasari

• Azimio wanashikilia kuwa Rais Ruto aliingia adarakani kwa njia isiyo halali na hata kwa njia hiyo wamekataa kusikiza vilio vya Wakenya na kutimiza ahadi walizowapa wakati wa kampeni.

 

Image: https://twitter.com/RailaOdinga/status

Sasa ni rasmi kwamba maandamano ya amani kushinikiza serikali ya Kenya Kwanza kushughulikia matakwa ya muungano wa Azimio yatang'oa nanga Machi 20.

Kiongozi wa Azimio Raila Odinga siku ya Alhamisi alitangaza kuwa maandamano  ya kitaifai yataanza rasmi Jumatatu, tarehe 20 mwezi Machi.

Odinga alitangaza haya katika mkutano wa viongozi wa Azimio waliojumuisha kinara wa Narc Kenya Martha Karua, Kalonzo Musyoka wa Wiper, Eugene Wanamalwa wa DAP na George Wajackoya wa Roots Party, miongoni mwa viongozi wengine.

Katika mkutano huo Raila pia alizindua vuguvugu la Movement for Defence of Democracy (MDD) alilosema litaendesha shughuli za kukomboa wakenya kutoka uongozi wa kiimla na usiojali maslahi ya wananchi chini ya Rais William Ruto. 

Muungano wa Azimio ulikuwa umeipa serikali ya Kenya Kwanza siku 14 kushughulikia matatizo yanayowakumba wakenya ikiwemo gharama ya juu ya maisha na uimarishaji wa uchumi, matakwa ambayo kulingana na Azimio hayakutimizwa.

 

Odinga alisema Wakenya wamebebeshwa mzigo mzito wa gharama ya juu ya maisha kutokana na bei ghali ya bidhaa muhimu, mafuta hali aliyosema ilisababishwa na hatua ya kuondolewa kwa ruzuku. Raila alisema ruzuku  iliwakinga wananchi dhidi ya gharama ya juu ya maisha.

"Tumeanzisha kampeni ya kwenda maandamano ya amani,kususia, kutotii na kuandamana ,"Bwana Odinga alisema

Wana Azimio wanashikilia kuwa Rais Ruto aliingia madarakani kwa njia ya mkato na kwa hivyo amekataa kusikiza vilio vya Wakenya na kutimiza ahadi alizotoa wakati wa kampeni.

Viongozi wengine wa Azimio waliunga mkono hoja za Raila . Kinara wa Narc Kenya Martha Karua ambaye alikuwa mgombeaji mwenza wake wakati wa kampeni alisema kuwa Ruto alichukua madaraka kimabavu hivyo basi  inabidi aondoke.

Kiongozi wa Wiper Kalonzo Musyoka amewahimiza wananchi kuitikia wito wa wa maandamano.