Naibu rais Rigathi Gachagua ndicho kikwazo cha umoja wa kitaifa - Savula

Savula alisema kuwa DP anapaswa kuacha tabia ya kujipiga kifua na na kuunganisha taifa.

Muhtasari

• Savula alisema kuwa Raila amezidisha upinzani wake dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza kwa sababu ya makabiliano ya mara kwa mara ya Gachagua.

Naibu gavana wa Kakamega Ayub Savula akiwahutubia wafuasi wake wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya Mpango wa Kaunti wa 'One Cow' mnamo Machi 14. Picha: HILTON OTENYO
Naibu gavana wa Kakamega Ayub Savula akiwahutubia wafuasi wake wakati wa uzinduzi wa awamu ya pili ya Mpango wa Kaunti wa 'One Cow' mnamo Machi 14. Picha: HILTON OTENYO

Naibu gavana wa Kakamega Ayub Savula amesema kuwa Naibu Rais Rigathi Gachagua ndiye wa kulaumiwa kwa hali ya kisiasa nchini kwa sasa.

Akihutubia wanahabari ofisini mwake Jumatano, Savula alisema kuwa DP anapaswa kuacha tabia ya kujipiga kifua na tabia ya kijambazi badala ya kuunganisha nchi.

"Tatizo katika nchi hii linatokana na DP ambaye ana shughuli nyingi za kuwatusi kiongozi wa Azimio Raila Odinga na rais mstaafu Uhuru Kenyatta. Viongozi hao wawili wana wafuasi wao ambao anawaudhi kwa kuwadhulumu viongozi wao. Baada ya uchaguzi unaunganisha nchi,” Savula alisema.

"Kama huwezi kutulia basi nyamaza. Kauli zako za kiholela zitateketeza nchi na nchi ikiungua tunaungua pamoja. Nina furaha kwamba rais William Ruto amepunguza semi zake kwa sababu anaelewa kuwa umoja wa nchi ni muhimu,” akaongeza.

Naibu gavana huyo alisema kuwa Raila amezidisha upinzani wake dhidi ya serikali ya Kenya Kwanza kwa sababu ya makabiliano ya mara kwa mara ya Gachagua.

Raila Jumanne alitangaza kuwa maandamano dhidi ya gharama ya juu ya maisha yatafanyika mara mbili kwa wiki kuanzia wiki ijayo, siku za Jumatatu na Alhamisi.

Naibu rais Rigathi Gachagua
Naibu rais Rigathi Gachagua
Image: Twitter

Ametangaza kuwa tume ya uchaguzi lazima ifungue seva zote ili kuthibitisha matokeo ya urais, kupunguza gharama ya maisha na kukubali kuwahusisha wahusika wote katika kuunda upya IEBC ili kukomesha maandamano hayo.

Savula wakati huo huo alisema kuwa Raila alikuwa akiwapa wafuasi wake matumaini kwa sababu hakuna njia ambayo anaweza kuandamana hadi Ikulu.

Alisema kuwa uchaguzi umekwisha na Mahakama ya Juu ilitangaza matokeo ya urais kuwa halali.

"Hakuna njia ya kisheria Raila anaweza kuingia ikulu isipokuwa atashiriki katika uchaguzi mkuu ujao," alisema.

Savula alisema kuwa nchi inahitaji mazungumzo ya kitaifa kuhusu kupanda kwa gharama ya maisha, na kuongeza kuwa hilo linaweza kufanywa tu na viongozi wenye akili timamu na si vitisho na majigambo kutoka pande zote mbili.

"Tunahitaji kama viongozi kufanya kazi kila saa ili kuwa na mazungumzo ya kitaifa ya jinsi ya kupunguza gharama ya maisha," alisema.

Alisema kuwa Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC) inabisha mlango ikiwa hali ya sasa ya kisiasa haitabadilika.

Alisema kuwa inasikitisha mtu wa hadhi ya naibu rais anaweza kuita serikali kampuni ya kibinafsi.

Alisema kuwa Wakenya wote wana haki ya kuishi nchini Kenya bila kujali wanaunga mkono upande gani wa kisiasa wakati wa uchaguzi mkuu.

TAFSIRI: DAVIS OJIAMBO.