Raila aonya Ruto na Gachagua kufuatia uvamizi wa mali za kibinafsi

Raila alisema rais Ruto na naibu wake Gachagua wanafaa kufahamu kuwa pia wao wana mali kote nchini.

Muhtasari

• Raila alidai kuwa uvamizi uliyotekelezwa katika shamba la Northlands na katika kampuni ya Spectre International ulifanyika chini ya maagizo ya rais Ruto na Gachagua.

KINARA WA AZIMIO RAILA ODINGA
Image: RAILA ODINGA/TWITTER

Kinara ya Azimio Raila Odinga ametoa onyo kali kwa rais William Ruto na naibu wake Rigathi Gachagua dhidi ya kuchochea uvamizi wa mali za watu binafsi.

Akihutubia wanahabari siku ya Jumanne Raila alisema rais Ruto na naibu wake Gachagua wanafaa kufahamu kuwa pia wao wana mali katika maeneo mbali mbali ya nchi.

Kiongozi huyo wa ODM alidai kuwa uvamizi uliyotekelezwa katika shamba la Northlands na katika kampuni ya Spectre International ulifanyika chini ya maagizo ya rais Ruto na Gachagua.

“Hakuna mtu atakaye dhani kwamba yuko salama nchini, mtu yeyote anayemiliki ardhi na mali atalengwa”, Raila alisema.

Polisi katika shamba la familia ya hayati mzee Uhuru Kenyatta kando ya Barabara ya Mashariki mnamo Machi 28, 2023 Picha: Bongo
Polisi katika shamba la familia ya hayati mzee Uhuru Kenyatta kando ya Barabara ya Mashariki mnamo Machi 28, 2023 Picha: Bongo

Raila vile vile alidai kuwa serikali ilifadhili makabiliano baina ya jamii mbili katika mtaa wa Kibra akisema kwamba mikutano ya kupanga mashambulizi hayo iliandaliwa katika boma la waziri mmoja wa zamani na mmoja ambaye bado anahudumu.

Kulingana na Raila vijana waliovamia shamba la familia ya Kenyatta na Spectre walisafirishwa kutoka maeneo ya Kayole na Nyeri kwa lengo la kuwaadhibu viongozi hao wawili ( Uhuru na Raila).

Alidai kuwa rais Ruto kupitia maagizo kwa idara ya polisi alikuwa kitekeleza mauaji ya wafuasi wa Azimio.

Kiongozi wa upinzani alipuuzilia mbali madai ya Inspekta Jenerali wa Police Japhet Koome kuwa maandamano yao yalikuwa kinyume cha sheria akisema kwamba idara ya polisi haina mamlaka kuharamisha maandamano yao.

“Koome alitumia sheria gani kupiga marufuku maandamano, Koome aliweka maaskari kuzuia Azimio kuingia mjini” Raila alisema.

Kinara huyo wa upinzami alidai kwamba walikuwa tayari wamejuwa mipango ya serikali kutumia baadhi ya maafisa wa polisi waliovalia nguo za raia katika mashambulizi.

Muungano wa Azimio vile vile ulikosoa jamii ya kimataifa kwa kusalia kimya huku unyama ukiendelea kutekelezwa dhidi ya wananchi wa Kenya.

Raila alisema hawasitisha maandamano yao hadi pale matakwa yao yatakapo shughulikiwa.

Maswala wanayotaka kutekelezwa ni; kupunguzwa kwa gharama ya maisha,kufunguliwa kwa sava za IEBC, kurejeshwa kwa makamishna wanne wa IEBC waliosimamishwa kazi na kushirikisha wadau wote katika harakati za kuunda upya tume ya IEBC.