Marekani yalaani mashambulizi dhidi ya wanahabari

Hili linajiri baada ya mashambulizi dhidi ya wanahabari wakati wa maandamano

Muhtasari

• Mashambulizi dhidi ya wanahabari yalianza wakati wa maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa Azimio Raila Odinga.

 

Balozi wa Marekani nchini Kenya Margaret Whitman wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Ubalozi wa Marekani, Gigiri mnamo Agosti 7, 2022.
Balozi wa Marekani nchini Kenya Margaret Whitman wakati wa mkutano na waandishi wa habari katika Ubalozi wa Marekani, Gigiri mnamo Agosti 7, 2022.
Image: MAKTABA

Serikali ya Marekani imeelezea wasiwasi wao  kuhusu uvamizi dhidi ya wanahabari ambao umekuwa ukiendelea kwa muda sasa tangu kuanza kwa maandamano.

Kupitia balozi wake nchini Kenya Meg Whitman, Marekani ilieleza kuwa  kuzingatia uhuru wa vyombo vya habari ni jambo la muhimu, na kwamba vyombo vya habari vina jukumu la kuendeleza demokrasia katika mataifa.

"Marekani ina wasiwasi mkubwa na ripoti za punde za mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari. Kulinda uhuru na usalama wa vyombo vya habari ni msingi wa demokrasia,' , alisema Whitman.

Hivi majuzi, mashambulizi dhidi ya wanahabari yamekuwa mengi, jambo linalotishia usalama wa waandishi wa habari.

Magenge yasiyojulikana yamekuwa yakishambulia magari ya wanahabari na hata visa vingi vya wanahabari walioumizwa kutokana na  mashambulizi haya vimeripotiwa.

Mashambulizi haya dhidi ya wanahabari yalianza wakati wa maandamano yaliyoitishwa na kiongozi wa Azimio ,Raila Odinga kupinga kupanda gharama ya maisha miongoni mwa mambo mengine mengi.

 

Baraza la vyombo vya Habari nchini Kenya (MCK), pia limekashifu vikali mashambulizi dhidi ya wanahabari likisema kuwa ni muhimu kuhakikisha vyombo vya habari vina uhuru wao kikamilifu.

Baraza hilo limesema kuwa Machi 2023 ni wakati  mgumu kwa vyombo vya habari tangu kupata demokrasia ya vyama vingi mwaka wa 1992.

MCK imesema kuwa imerekodi visa 25 vya mashambulizi dhidi ya wanahabari wakati wa maandamano.