Trump kushtakiwa kwa kununua kimya cha muigizaji wa filamu za utupu

Yeye ndiye rais wa kwanza au rais wa zamani wa Marekani kukabiliwa na mashtaka ya jinai.

Muhtasari

• Trump alimlipa Stormy Daniels katika jaribio la kununua kimya chake kuhusu madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi.

• Rais huyo wa zamani, anayeishi Florida, anatarajiwa kusafiri hadi New York siku ya Jumatatu na kufikishwa mahakamani Jumanne.

• Idara ya Huduma ya Siri ya Marekani - ambayo ina jukumu la kuwalinda marais wanaohudumu na marais wa zamani wa Amerika - itasimamia usalama wa kesi hiyo.

Image: GETTY IMAGES

Rais wa zamani wa Marekani Donald Trump atashtakiwa kwa malipo ya kimyakimya yaliyotolewa kwa nyota wa filamu za ngono kabla ya uchaguzi wa urais wa 2016.

Maelezo ya kesi dhidi yake bado hayajatolewa.

Baraza kuu la mahakama limepiga kura kumfungulia mashtaka baada ya kuchunguza malipo ya $130,000 kwa Stormy Daniels katika jaribio la kununua kimya chake kuhusu madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi.

Bw Trump, 76, anakanusha kufanya makosa. Yeye ndiye rais wa kwanza au rais wa zamani wa Marekani kukabiliwa na mashtaka ya jinai.

Ofisi ya Wakili wa Wilaya ya Manhattan, Alvin Bragg, ambaye amekuwa akifuatilia uchunguzi huo, ilithibitisha kwamba iliwasiliana na wakili wa Bw Trump ili "kuratibu kujisalimisha kwake" kwa mashtaka ambayo hayakutajwa.

Rais huyo wa zamani, anayeishi Florida, anatarajiwa kusafiri hadi New York siku ya Jumatatu na kufikishwa mahakamani Jumanne, vyanzo viwili vinavyofahamu suala hilo viliiambia CBS News, mshirika wa BBC wa Marekani.

Mashtaka katika hati ya mashitaka yatasomwa kwake kwenye usikilizwaji wa kesi hiyo, ambayo itadumu kama dakika 10-15.

Idara ya Huduma ya Siri ya Marekani - ambayo ina jukumu la kuwalinda marais wanaohudumu na marais wa zamani wa Amerika - itasimamia usalama wa kesi hiyo.

Bw Trump anakabiliwa na uwezekano wa kurekodiwa alama za vidole na kupigwa picha , kama washtakiwa wote katika kesi za uhalifu.

Katika taarifa, Bw Trump alimsuta wakili wa wilaya ya Manhattan. Alimwita mwendesha mashtaka huyo kama "fedheha", na kumshutumu kwa "kufanya kazi chafu ya Joe Biden".

Image: GETTY IMAGES

Wanachama wa democrats wamesema uwongo, wamedanganya na kuiba kwa shauku yao ya kujaribu 'Kumpata Trump,' lakini sasa wamefanya jambo lisilofikirika - kumfungulia mashtaka mtu asiye na hatia kabisa kwa kitendo cha kuingiliwa wazi kwa Uchaguzi," alisema.

Bw Trump amekashifu mara kwa mara uchunguzi huo katika mji alikozaliwa wa New York kama "hila" ya kisiasa inaoongozwa na wapinzani wake.

Bw Bragg, ambaye amesajiliwa kutoka chama cha Democrat, amekanusha kuwa ana mpango wa kisasi dhidi ya Bw Trump. "Tunatathmini kesi katika mamlaka yetu kwa kuzingatia ukweli, sheria, na ushahidi," aliandika kwenye Twitter mapema mwezi huu.

Wakili wa Bw Trump, Susan Necheles, alisema katika taarifa yake: "Hakufanya uhalifu wowote. Tutapambana vikali na mashtaka haya ya kisiasa mahakamani."

Uchunguzi huo unatokana na madai kwamba Bw Trump alimwagiza wakili wake wakati huo Michael Cohen amlipe Stormy Daniels, mwigizaji wa zamani wa filamu za utupu chini ya wiki mbili kabla ya uchaguzi wa urais wa 2016 ili kumzuia asizungumze kuhusu madai ya kuwa na uhusiano wa kimapenzi na Bw Trump.

Bi Daniels amesema alifanya mapenzi na Bw Trump katika hoteli ya Lake Tahoe mwaka wa 2006 - mwaka mmoja baada ya kuoa mke wake wa sasa, Melania.

Cohen amesema mahakamani kwamba alifanya malipo ya $130,000 "kwa uratibu na kwa maelekezo ya" rais huyo wa zamani. Cohen alifungwa kutoka 2018-2020 kwa mashtaka mengi.

Kufuatia kufunguliwa mashtaka, Bi Daniels aliwashukuru wafuasi wake. "Nina jumbe nyingi zinazoingia ambazo siwezi kujibu...pia sitaki kumwaga shampeni yangu," aliandika Twitter

Image: REUTERS

Kesi hiyo ya jinai inaweza kubadilisha kinyang'anyiro cha urais 2024. Bw Trump kwa sasa ndiye mshindani wa aliye mstari wa mbele kati ya wote waliotangazwa na wanaotarajiwa kuwania uteuzi wa chama cha Republican White House.

Lakini hakuna chochote katika sheria za Marekani kinachomzuia mgombea anayepatikana na hatia ya uhalifu kufanya kampeni, na kuwa rais - hata kutoka gerezani.

Kampeni yake ilituma barua pepe za kuchangisha pesa Alhamisi jioni, akitoa mfano wa mashtaka.

Wabunge wakuu wa chama cha Republican wanamuunga mkono Trump.

Spika wa Baraza la Wawakilishi Kevin McCarthy alisema: "Alvin Bragg ameharibu nchi yetu kwa njia isiyoweza kurekebishwa katika jaribio la kuingilia uchaguzi wetu wa Urais.

"Anapowaachilia mara kwa mara wahalifu wa jeuri ili kuwatishia umma, aliutumia mfumo wetu mtakatifu wa haki dhidi ya Rais Donald Trump."

Lakini Wanademokrasia walikaribisha shtaka hilo, wakisema ilionyesha hakuna mtu aliye juu ya sheria.

Mbunge Adam Schiff alisema: "Kushtakiwa na kukamatwa kwa rais wa zamani ni wa kipekee katika historia yote ya Marekani

"Lakini pia ni tabia isiyo halali ambayo Trump ameshtakiwa."

Bw Trump pia anachunguzwa katika visa vingine kadhaa.

Ni pamoja na uchunguzi kuhusu jukumu lake katika ghasia za Bunge la Marekani la Januari 2021, juhudi zake za kubatilisha kushindwa kwake katika jimbo la Georgia katika uchaguzi wa 2020, na utunzaji wake wa hati za siri baada ya kuondoka madarakani.

Bw Trump - ambaye alihudumu kama rais kutoka 2017-2021 - alishtakiwa mara mbili na Baraza la Wawakilishi. Aliachiliwa na Seneti mara zote mbili.