Mmoja afariki, 23 wajeruhiwa huku magari yakiteketea Mombasa Road

Basi la abiria na gari la Toyota Hilux ziligongana uso kwa uso kabla ya kuteketea Ijumaa usiku.

Muhtasari

•Napeiyan alisema mtu aliyefariki ni dereva wa Toyota Hilux huku majeruhi wakiwa ni abiria waliokuwa ndani ya basi.

•Dereva wa Pickup alichomwa moto kiasi cha kutotambulika.

ambayo yaliteketea kwa moto kando ya barabara ya Mombasa katika eneo la Maanzoni Lodge huko Athi River, Kaunti ya Machakos mnamo Ijumaa, Aprili 21, 2023.
Magari mawili ambayo yaliteketea kwa moto kando ya barabara ya Mombasa katika eneo la Maanzoni Lodge huko Athi River, Kaunti ya Machakos mnamo Ijumaa, Aprili 21, 2023.
Image: GEORGE OWITI

Mtu mmoja amefariki huku wengine 23 wakipata majeraha mabaya baada ya magari mawili kuwaka moto katika barabara ya Mombasa.

Mkuu wa polisi katika Kaunti ya Machakos Joseph Ole Napeiyan alisema basi la abiria na gari la Toyota Hilux ziligongana uso kwa uso kabla ya kuteketea kwa moto Ijumaa usiku.

Ajali hiyo, kulingana na Napeiyan, ilitokea kwenye barabara kuu ya Nairobi - Mombasa karibu na kituo cha mafuta cha Shell, mita chache kutoka Maanzoni Lodge, eneo la Athi River, Kaunti ya Machakos mwendo wa saa saba usiku wa kuamkia Ijumaa. 

Kisa hicho kiliripotiwa katika kituo cha polisi cha Kyumbi eneo la Makutano Junction, Kaunti ya Machakos.

Napeiyan alisema mtu aliyefariki ni dereva wa Toyota Hilux huku majeruhi wakiwa ni abiria waliokuwa ndani ya basi.

Marehemu hakutambuliwa mara moja.

"Toyota Hilux iliyokuwa ikielekea Nairobi iligongana uso kwa uso na gari lililokuwa likija," Napeiyan alisema.

Alisema kutokana na hali hiyo, dereva wa pickup alinaswa ndani ya gari hilo ambalo liliwaka moto. Alichomwa moto kiasi cha kutotambulika.

“Dereva wa basi na abiria walijeruhiwa baada ya magari hayo kuwaka moto. Moto huo ulizimwa na kikosi cha wazima moto kutoka serikali ya Kaunti ya Machakos,” Napeiyan alisema.

Mkuu huyo wa polisi alisema majeruhi wote walikimbizwa katika hospitali ya Machakos Level 5 na wanaendelea na matibabu huku marehemu akipelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti akisubiri kufanyiwa uchunguzi na kutambuliwa.

Mabaki ya magari yalivutwa hadi kituo cha polisi cha Kyumbi kwa ukaguzi.

Napeiyan alisema maafisa kutoka idara ya trafiki kituo cha polisi cha Kyumbi wameanzisha uchunguzi kuhusu ajali hiyo.

Aliwaonya madereva dhidi ya kukiuka sheria za trafiki ili kupunguza visa vya ajali.