Msichana wa gredi ya 3 akufa maji Suba Kaskazini

Wakazi walisema msichana huyo wa umri wa miaka 12 aliteleza ndani ya mto alipokuwa akichota maji.

Muhtasari
  • Mwanafunzi huyo wa darasa la 3 alizama kwenye mto Gendo Kibwer Jumapili jioni
  • Alikuwa pamoja na ndugu zake wawili wakati tukio hilo lilipotokea.
Crime Scene
Image: HISANI

Familia moja katika kijiji cha Gendo eneo bunge la Suba Kusini inaomboleza baada ya binti yao kufa maji alipokuwa akichota maji.

Mwanafunzi huyo wa darasa la 3 alizama kwenye mto Gendo Kibwer Jumapili jioni.

Wakazi walisema msichana huyo wa umri wa miaka 12 aliteleza ndani ya mto alipokuwa akichota maji.

Alikuwa pamoja na ndugu zake wawili wakati tukio hilo lilipotokea.

“Msichana huyo alikuwa akichota maji ya kufulia nguo. Aliteleza kabla ya kuzama,” mkazi mmoja alisema.

Akizungumza siku ya Jumatatu kuhusu suala hilo, chifu wa Gwasi Mashariki Andrew Ombisa alisema mto huo ulikuwa umefurika kutokana na mvua inayoendelea kunyesha.

Alisema kutokana na mvua hizo ndefu, mito imevunja kingo zake.

Msichana huyo alitakiwa kurejea shuleni Jumatatu kwa muhula wa pili.

“Kwa bahati mbaya aliteleza na kuzama mtoni. Familia yake imeshangazwa na kifo hicho cha ghafla,” Ombisa alisema.

Ndugu zake walipiga kelele na kusababisha wakazi kukimbilia eneo la tukio.

Ombisa alisema hawakumpata msichana huyo mara baada ya kuzama.

Mwili huo ulitolewa baada ya saa mbili.

Msimamizi huyo alitoa wito kwa wazazi kuwa macho ili kujua waliko watoto wao.

"Tunawasihi wazazi kuwatunza watoto wao. Wanapaswa kufuatilia mienendo yao,” Ombisa alisema.

Mwili huo ulihamishiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya St Camillus katika mji wa Sori.