Rais Ruto anaonekana kuishi dunia nyingine arejeshwe - Raila

Raila alidai kuwa Ruto anajaribu kubadilisha kiwango cha juu cha deni la nchi kutoka trilioni 10 hadi asilimia 55 ya Pato la Taifa.

Muhtasari

• Kiongozi huyo wa upinzani alitoa wito kwa wakenya kukataa ushuru uliopendekezwa ili kuokoa uchumi wa nchi.

KINARA WA MUUNGANO WA AZIMIO RAILA ODINGA
Image: TWITTER

Kiongozi wa Azimio la Umoja Raila Odinga amesema Rais William Ruto anaonekana kutojua au kuguswa na hali ya sasa nchini.

Kulingana Raila, hata kama rais anaendelea kupendekeza nyongeza ya ushuru, anaonekana kutohisi mateso ya Wakenya.

"Ni haraka tumrejeshe Ruto duniani kwa sababu anaishi katika sayari nyingine," Raila alisema.

Alizungumza Alhamisi jijini Nairobi na kudai kuwa serikali ya Rais Ruto imekopa pesa nyingi kuliko serikali nyingine yoyote, lakini huduma nyingi za serikali hazijakuwa zikitolewa.

"Wameondoa ruzuku, wamepandisha ushuru lakini uhaba wa pesa umeendelea. Hawawezi kulipa mishahara. Hawawezi kutoa pesa shuleni. Hawawezi kutoa pesa kwa kaunti,” Raila alisema.

“Hawawezi kutoa pesa kwa wazee, hawawezi kufadhili NHIF. Na karibu miradi yote mikubwa ya miundombinu imekwama. Pesa zinakwenda wapi?"

Raila alidai kuwa Ruto anajaribu kubadilisha kiwango cha juu cha deni la nchi kutoka kiwango cha sasa cha shilingi trilioni 10 hadi asilimia 55 ya Pato la Taifa.

"Kiwango cha deni tayari ni asilimia 60 ya Pato la Taifa Ili kukwepa sheria, Ruto anataka kulazimisha marekebisho ya Sheria ya Fedha za Umma ili kuruhusu wizara ya fedha kuamua kiwango cha deni la Kitaifa na wala si Bunge,” Raila alisema.

Kiongozi huyo wa upinzani alitoa wito kwa wakenya kukataa ushuru uliopendekezwa ili kuokoa uchumi wa nchi.

“Mswada huu unapoelekea katika Bunge la Kitaifa, lazima tumkumbushe Ruto kwamba ushuru kupita kiasi unatatiza ukuaji. Ni lazima tumwambie Ruto kwamba watu wanapolazimika kuegesha magari nyumbani na kuahirisha safari za mashambani kwa sababu hawawezi kumudu mafuta au nauli, ni mbaya kwa uchumi,” Raila alisema.