Nairobi: Watu 10 wakamatwa kwa kupiga picha bila idhini kwenye majumba ya kifahari

Serekali yaanza oparesheni ya kusaka waahalifu

Muhtasari

• Polisi wanasema wameongeza ufuatiliaji na doria kama sehemu ya juhudi za kudhibiti mashambulizi yanayohusiana na ugaidi.

polisi wakamata watu kumi kwa tuhuma za kupiga picha
Pingu polisi wakamata watu kumi kwa tuhuma za kupiga picha
Image: Radio Jambo

Polisi  walikamata  watu kumi ambao walituhumiwa kupiga picha kwenye maduka makubwa.

Baadhi walikamatwa katika  jumba la GTC Mall huku wengine wakiwa kwenye bwawa la kuogelea ndani ya mgahawa wa GTC wakipiga picha zikiwemo picha ya selfie.

Walisindikizwa hadi kituo cha polisi cha Parklands kwa mahojiano kabla ya kuachiliwa.

Polisi pia waliitwa katika jumba la maduka la Westgate lililo karibu ambapo waliwazuilia raia wa  kigeni wengine waliokuwa wakipiga picha.

 

Haya yanajiri kufuatia kumalizika kwa miaka 10 ya  shambulio la Westgate Mall ambalo lilisababisha vifo vya watu 71 na wengine kadhaa kujeruhiwa.

Polisi wanasema wameongeza ufuatiliaji na doria kama sehemu ya juhudi za kudhibiti mashambulizi yanayohusiana na ugaidi.

Afisa mkuu alisema hatua ya walinzi katika maduka hayo kuita polisi ni ishara ya tahadhari na umakini.

"Wengine wanaweza kuona kuwa ni unyanyasaji lakini chochote walichofanya kilikuwa sehemu ya juhudi za kuhakikisha usalama wetu kwa ujumla," polisi walisema.

  Maeneo ambayo kupiga picha ni marufuku ni pamoja na mitambo ya kijeshi, viwanja vya ndege na majengo ya serikali, mbuga za wanyama, mali ya kibinafsi na majengo nyeti ya serikali ikiwa ni pamoja na vituo vya polisi, magereza na vituo vingine vya serikali.

Baadhi ya sheria zilizopo zinazosimamia upigaji picha ni pamoja na Sheria ya Siri Rasmi, Sura ya 187 inayokataza upigaji picha au kutengeneza michoro au mipango ya maeneo maalum, kama vile mitambo ya kijeshi, majengo ya serikali na maeneo mengine nyeti.

Sheria hii inalenga kulinda usalama wa taifa na kuzuia ufichuzi wa siri za serikali. Sheria ya Maeneo Tengefu na Uhifadhi wa Wanyamapori, Sura ya 376 inakataza upigaji picha katika baadhi ya maeneo yaliyohifadhiwa, kama vile mbuga za wanyama na hifadhi za wanyamapori, bila kibali.