Waziri wa kawi Davis Chirchir amruka Ann Njeri kuhusu shehena ya dizeli

Waziri alidai kuwa Njeri alikosa kufikia kiwango cha chini zaidi cha kupata leseni ya kuagiza mafuta na stakabadhi alizotumia kudai shehena ni ghushi.

Muhtasari

• Chirchir alisema madai ya Njeri kwamba alipata leseni ya kuagiza mafuta kutoka kwa Epra, alilipia na alikuwa akingojea tu kutiwa saini ni uzushi usio wa kweli na kamili.

Waziri wa kawi Davis Chirchir
DAVIS CHIRCHIR Waziri wa kawi Davis Chirchir
Image: EZEKIEL AMING'A

Waziri wa Kawi Davis Chirchir sasa anadai kuwa mfanyabiashara Ann Njeri aliwasilisha hati ghushi ambazo alitaka kudai tani 93,000 za dizeli kutoka Saudi Arabia.

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, Waziri alitoa msururu wa matukio yaliyopelekea kuingizwa na hatimaye kutolewa kwa shehena hiyo katika Kituo cha Kuhifadhi Mafuta cha Kipevu mnamo Novemba 4.

Alikanusha madai ya mfanyabiashara huyo kwamba yeye ndiye mwagizaji halisi wa shehena hiyo akisema ombi lake la leseni ya kuagiza mafuta lilikataliwa Oktoba 29 na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Petroli (Epra).

"Anns Import and Export Enterprises Limited kwa hivyo haina leseni ya kuagiza mafuta ya petroli nchini Kenya kama inavyotakiwa chini ya Kifungu cha 74(1)(a) cha Sheria ya Petroli ya 2019 na kwa hivyo haiwezi kudai kuwa iliingiza shehena ya dizeli nchini kwa MT Haigui," Chirchir alisema.

Alisema Njeri alikosa kufikia kiwango cha chini zaidi cha kupata leseni ya kuagiza bidhaa na stakabadhi alizotumia kudai shehena ya mafuta zote ni ghushi.

Chirchir alisema madai ya Njeri kwamba alipata leseni ya kuagiza mafuta kutoka kwa Epra, alilipia na alikuwa akingojea tu kutiwa saini ni uzushi usio wa kweli na kamili.

“Kwanza, Epra kwa sasa haitozi ada za leseni za mafuta ya petroli na pili, Epra haina ndani ya kumbukumbu zake leseni ya uagizaji wa mafuta ya petroli iliyotolewa kwa kampuni ya Anns Import and Export Enterprises Limited ambayo inasubiri kusainiwa,” alisema.

Kulingana na CS, msimamo wa kweli ni kwamba shehena ya mafuta iliagizwa na Aramco Trading Fujairah FZE kupitia Galana Energies Limited.

Alisema Galana ilifuata utaratibu wa kisheria wa uingizaji wa tani 93,460.46 za shehena ya dizeli KG 22/2023 ikiwa na stakabadhi zote.

"Msimamizi wa meli alikataa stakabadhi za Kupakia zilizotolewa na kampuni ya Anns Import and Export Enterprises Limited akisema ni ghushi," Chichir alisema.

Alisema sababu za stakabadhi za Njeri kuwa ghushi ni kwamba zilikuwa na mhuri usiyofanana na mhuri wa MT Haigui na zilikuwa na idadi isiyo sahihi ya shehena. 

"Ni vyema kufahamu kwamba stakadhi ya Kupakia iliyotolewa na kampuni ya Anns Import and Export Enterprises Limited ilikuwa ya tarehe 9 Oktoba 2023, lakini MT Haigui ilifika katika Bandari ya Mombasa mnamo Oktoba 11, 2023, na hivyo kufanya iwe vigumu kwa meli kusafiri kutoka Saudi, Uarabuni ndani ya siku mbili tu." 

Akiongea na Wanahabari Jumanne nje ya Mahakama Kuu ya Mombasa, Njeri alishikilia kuwa yeye ndiye mmiliki halali wa tani 100,000 za shehena ya dizeli yenye thamani ya Sh17 bilioni. 

Alizungumza baada ya kuibuka tena kufuatia siku kadhaa za uvumi kuhusu aliko tangu Alhamisi wiki jana baada ya kurekodi taarifa katika makao makuu ya DCI kuhusu mzozo huo wa mafuta. 

"Nilikuwa nikisubiri kibali changu cha kuagiza na kwenda kuonana na CS Chirchir ambaye aliniambia mafuta sio yangu bali ni ya kampuni moja iitwayo Galana, nikamwambia sijasaini mkataba wowote na Galana, hivyo mizigo ni yangu. Akanishauri. niende kwa DCI kurekodi taarifa,” alisema. 

Kulingana na Njeri, alichukuliwa kutoka kwa afisi za DCI na wanaume alioamini kuwa ni maafisa na kupelekwa mahali pasipojulikana huku akiwa amezibwa macho na kuhojiwa usiku kucha. 

“Niliwaambia mafuta ni yangu na nyaraka zote ninazo, wakaniambia hawakuona kosa na kwamba mafuta ni yangu kweli, wakanifunga macho na tukaondoka nyumbani, wakanitupa Nyayo Estate. ," alisema. 

Siku ya Jumatatu, mwenyekiti wa Mamlaka ya Bandari ya Kenya Benjamin Tayari na mkurugenzi mkuu Kapteni William Ruto walidai kuwa hati za Njeri ni ghushi.