Francis Atwoli atangaza mabadiliko mapya kwenye uongozi wa muungano COTU

Kasisi Joel Kandie ndiye Mwenyekiti Mkuu mpya wa bodi ya wafanyakazi

Muhtasari

•Katibu Atwoli aliwasihi maafisa wapya waliochaguliwa kuendelea kupigania uboreshaji wa haki na ustawi wa wafanyikazi wa Kenya

Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli
Katibu mkuu wa COTU Francis Atwoli

Katibu Mkuu wa Muungano wa Vyama vya Wafanyakazi nchini (COTU) Francis Atwoli ametangaza kuchaguliwa kwa Kasisi,Joel Kandie Chebii kuwa Mwenyekiti Mkuu mpya wa bodi ya wafanyakazi.

Atwoli, katika taarifa yake kwa vyumba vya habari  alisema kuwa Kandie ametumikia COTU kwa miongo minne iliyopita.

Kuchaguliwa kwa Kandie na Halmashauri Kuu ya COTU kunafuatia kifo cha Mwenyekiti Mkuu wa muda mrefu Rajabu Wellington Mwondi aliyefariki akitibiwa katika Hospitali ya Aga Khan mjini Kisumu Agosti mwaka huu.

Atwoli vile vile alitangaza kuwa Wycliffe Nyamwatta, ambaye amehudumu katika bodi ya COTU kwa miongo miwili, pia alichaguliwa kuwa Makamu Mwenyekiti Mkuu wa pili wa chama cha wafanyakazi.

Katibu Atwoli aliwasihi maafisa wapya waliochaguliwa kuendelea kupigania uboreshaji wa haki na ustawi wa wafanyikazi wa Kenya.

"Utulivu ni muhimu kwa mashirika yote ikiwemo hii  COTU tutaendelea kuhakikisha kuwa Muungano una umoja na utulivu ili kuhudumia wafanyikazi wa Kenya," alisema.