Familia ya Jowie yavunja kimya kufuatia hukumu ya kifo

"Binafsi ninaamini kuwa mwanangu hana hatia, na hajafanya kosa lolote, hajaua," mamake Jowie alisema.

Muhtasari

•Familia ya Jowie Irungu imeshikilia kuwa mfungwa huyo mwenye umri wa miaka 33 hana hatia na hakumuua mfanyibiashara Monica Irungu.

•Mamake Jowie alisema imani kuwa mwanawe hatimaye atatoka tena ndiyo inampa nguvu.

mnamo siku ya hukumu, Machi 13, 2024.
Jowie Irungu akiwa pamoja na dadake, mamake na babake mnamo siku ya hukumu, Machi 13, 2024.
Image: HISANI

Familia ya mfungwa Joseph Irungu almaarufu Jowie imeshikilia kuwa mfungwa huyo mwenye umri wa miaka 33 hana hatia na hakumuua mfanyibiashara Monica Irungu.

Mamake Jowie, Bi Anastacia Thama, ambaye alizungumza na waandishi wa habari nje ya mahakama ya Milimani siku ya Jumatano alionyesha imani kubwa na mwanawe akisema hakutenda kosa lolote ili kustahili hukumu ya kifo aliyopewa.

"Binafsi ninaamini kuwa mwanangu hana hatia, na hajafanya kosa lolote, hajaua," Bi Thama alisema.

Alionyesha imani yake kwamba mwanawe bado ana nafasi nyingine ya uhuru, akisema kwamba kuamini kuwa hatimaye atatoka tena ndilo jambo linalompa nguvu.

“Kuna kitu nina amini, kuna Mungu wa nafasi nyingine, na atamtoa. Na ndio maana mnaona niko na nguvu hivi, kwa sababu Mungu ambaye ninaamini, ndiye atamtoa,” alisema.

Aliongeza, “Yeye ni kama Joseph, Joseph alidhulumiwa hivi na Mungu baadaye alimtoa. Na hata mimi naamini atamtoa.”

Baba na dada wa mfungwa pia walikuwepo wakati wa hukumu hiyo.

Wakili wa Jowie alibainisha kuwa wako tayari kukata rufaa dhidi ya hukumu hiyo kwani bado wanaamini kuwa hana hatia.

Jowie bado ana fursa ya kujinusuru dhidi ya hukumu ya kunyongwa.

Mfungwa huyo sasa ana siku kumi na nne baada ya kuhukumiwa za kuwasilisha rufaa dhidi ya hukumu ya kifo ambayo alipewa siku ya Jumatano. 

Jaji Grace Nzioka alitoa hukumu hiyo katika Mahakama ya Milimani siku ya Jumatano alasiri kufuatia hukumu ya hatia iliyotolewa mnamo Februari 9, 2024. Mtuhumiwa alipatikana na hatia ya kumuua mfanyibiashara Monica Kimani mnamo Septemba 2018.

Wakati akitoa hukumu, Jaji Grace Nzioka alibainisha kuwa mshtakiwa hana sifa ya kutumikia kifungo cha nje.

“Kwa kuzingatia yote nimesema, kwa hivyo, ninaamuru kwamba mshtakiwa wa kwanza Joseph Kuria Irungu almaarufu Jowie amehukumiwa kunyongwa kama ilivyoelezwa kwa kosa la mauaji chini ya kifungu cha 204 cha kanuni ya adhabu ya Kenya isipokuwa hukumu hiyo itolewe kando na mahakama yenye mamlaka," Jaji Nzioka alisema.

Hukumu hiyo ilitolewa baada ya mahakama kumpata Jowie na hatia ya mauaji ya Monica Kimani.

Mahakama iligundua kuwa mfanyibiashara huyo mwenye umri wa miaka 28 hakufa kifo cha kawaida, bali aliuawa kama ilivyothibitishwa na upande wa mashtaka.

Hukumu ya Jowie jela inamaliza kesi ya mauaji ambayo imekuwa ikiendelea kwa miaka sita iliyopita.