Mwanamume aliyejihami kwa panga aingia kituo cha polisi Muranga na kuwashambulia maafisa

Afisa mmoja alijikinga kutumia mkono wake na kusababisha kidole cha kati kukatwa huku kidole cha pili kikijeruhiwa vibaya.

Muhtasari

•Mshukiwa anasemekana kuvamia kituo cha polisi cha Nyakahura, katika kaunti ndogo ya Kangema kuripoti mzozo wa ardhi na jirani yake.

•Maafisa hao wawili kwa sasa wanapokea matibabu katika hospitali ya kibinafsi ya Murang'a na wako katika hali nzuri.

Crime scene
Crime scene
Image: HISANI

Mwanamume mmoja amekamatwa mjini Murang'a kwa madai ya kuwashambulia maafisa wawili wa polisi kwa panga.

Mshukiwa anasemekana kuvamia kituo cha polisi cha Nyakahura, katika kaunti ndogo ya Kangema kuripoti mzozo wa ardhi na jirani yake.

Lakini huku akiongozwa na afisa wa zamu, James Gitonga, kuhusu jinsi ya kushughulikia suala hilo, mshukiwa anasemekana kutoa panga alilokuwa ameficha na kumvamia afisa huyo wa zamu.

"Ghafla alitoa panga alilokuwa ameficha na kulenga kichwa cha afisa," ripoti ya polisi iliyofikia Radio Jambo ilisoma

Afisa huyo alijikinga kwa kutumia mkono wake na kusababisha kidole chake cha kati kukatwa huku kidole cha pili kikijeruhiwa vibaya.

"Baada ya kushambuliana, mshambuliaji alikimbia na msako ukafuata. Katika harakati hizo, mshukiwa alimgeukia afisa mwingine aliyetambulika kwa jina la John Kimathi na kumkata vibaya mkono wa kushoto na upande wa kulia wa kifua," ripoti ya polisi iliongeza.

Maafisa hao wawili kwa sasa wanapokea matibabu katika hospitali ya kibinafsi ya Murang'a na wako katika hali nzuri.

Mshukiwa mwenye umri wa miaka 59 yuko chini ya ulinzi wa polisi.