Mtoto mwenye ualbino aibwa, Polisi yafanya msako

Kanda ya ziwa Victoria bado imeendelea kuwa eneo ambalo kuna matukio ya ukatili kwa watu wenye ualbino.

Muhtasari

• Matukio ya namna hiyo pia yamekuwa yakiripotiwa katika nchi Jirani ya Malawi.

• Chama cha watu wenye Ualbino nchini Tanzania kinasema kimeshtushwa na tukio la kuibwa kwa mtoto mwenye ualbino.

• Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Blacius Chatanda aliiambia BBC kuwa bado wanamtafuta mtoto huyo huku uchunguzi ukiwa bado unaendelea.

Image: BBC

Chama cha watu wenye Ualbino nchini Tanzania kinasema kimeshtushwa na tukio la kuibwa kwa mtoto mwenye ualbino, Asiimwe Novath wa umri wa miaka miwili na nusu. Asiimwe alichukuliwa nyumbani kwao kaskazini magharibi mwa nchi hiyo katika kijiji cha Bulamula, kata ya Kamachumu, wilayani Muleba mkoani Kagera Mei 30 majira ya saa mbili usiku.

Kwa takriban miaka kumi sasa, matukio ya mauaji ya watu wenye ualbino yalipungua kwa kiasi kikubwa. Sasa kutekwa kwa mtoto Asiimwe kumeishtua jamii.

Mwenyekiti wa Chama Cha Watu wenye Ualbino Tanzania, Godson Solomon Mollel anasema wameshtushwa na kusikitishwa na tukio hilo.

Kamanda wa Polisi Mkoani Kagera, Blacius Chatanda aliiambia BBC kuwa bado wanamtafuta mtoto huyo huku uchunguzi ukiwa bado unaendelea.

Alisema wanawashikilia watu watatu kuhusiana na kuibwa kwa mtoto Asiimwe. Amewataja wanaoshikiliwa kuwa ni baba wa mtoto na watu wengine wawili ambao hawana uhusiano na mtoto, japo hakuwataja majina yao. Pia aliznguzmzia matuko ya aiana hiyo mkaoni Kagera.

”Matukio haya kwa mkoa wa Kagera hayajazoeleka lakini pia mikoa mingine ambayo matukio kama haya yalikuwa yanatokea kwa kipindi kirefu yalikuwa yamepotea. Kimsingi tukio hili kwa Kagera limevuta hisia za wananachi wengi hasa wananchi wema wamechukizwa na tukio la namna hiyo, kimsingi hakuna mtu ambaye anaweza kufurahia tukio la namna hii’

Kanda ya ziwa Victoria bado imeendelea kuwa eneo ambalo kuna matukio ya ukatili kwa watu wenye ualbino. Mollel anasema ni ndani ya mwezi mmoja tu uliopita tukio la kikatili dhidi ya mtoto mwenye ualbino lilitokea mkoani Geita.

‘Kwa kuchukuliwa mtu hadharani, tukio la Geita ndilo tungelifananisha na hilo ambalo mtoto Kazungu Julius alikatwa mkono wake na kichwa na bega’.

Baada ya tukio hili la mtoto Asiimwe, polisi mkoani Kagera wanasema wameimarisha ushirikiano na wananchi kupata taarifa za wahalifu kwa haraka na kuimarisha ulinzi kwa watu wenye ualbino.

‘Kwa Kagera hili ndiyo limetokea, lakini sidhani kama yanaweza kutokea matukio mengine ya namna hiyo kwa mkoa huu kwa sababu polisi ipo karibu sana na wananchi na imejikita sana kwa polisi jamii na ile miradi yake lakini, kata zote zina wagakuzi kata na askari kata na vikundi shirikishi, kwa ujumla wananchi wamaeneo haya wamejipanga vizuri kwa sasa’

Miaka kumi iliyopita, juhudi kubwa zilifanywa kukamata wahalifu na kutoa elimu kwa umma kukabiliana na mauaji haya ya kikatili. Mathalani mwanzoni mwa mwaka 2015, zaidi ya waganga wa jadi 200 walikamatwa, wakihusishwa na mauaji haya ya kinyama. Kuibuka kwa matukio haya mapya kunaashiria uhitaji tena kwa jamii na vyombo vya ulinzi na usalama kuimarisha ulinzi na usalama wa watu wenye ualbino Tanzania.

Matukio ya namna hiyo pia yamekuwa yakiripotiwa katika nchi Jirani ya Malawi.