Mwanamume aliyemshambulia polisi ahukumiwa miaka saba

Kasesi mwenye miaka 24 alimshambulia afisa huyo akiwa kazini

Muhtasari

•Afisa huyo alidhulumiwa akiwa kazini kiasi cha kumfanya auguze majeraha 

•Awali Kasesi alikataa kujibu mashtaka kwa nyakati mbili tofauti kabla ya kukiri mashtaka yote manne aliyokabiliwa nayo

•Hakimu alibainisha kuwa kosa la kuwashambulia askari polisi linazidi kukithiri nchini hivyo basi kifungo hicho kitakuwa kama mfano kwa wengine

Mwanamke aliyefungwa jela pingu mikononi.
Mwanamume aliyemshambulia polisi ahukumiwa Mwanamke aliyefungwa jela pingu mikononi.
Image: Shutterstock

Mwanamume wa miaka 24 , Tyson Kasesi, amehukumiwa kifungo cha miaka saba gerezani baada ya kupatikana na kosa la kumshambulia afisa wa polisi akiwa kazini.

Inasemekana, Kasesi alimshambulia afisa huyo kwa kumpiga na kumdhulumu afisa wa mwezi Mei mwaka huu katika kaunti ya Kakamega.

Tyson Kasesi aliripotiwa kutenda kosa hilo ambalo ni kinyume na kifungu cha 103(a) cha Sheria ya Kitaifa ya Polisi.

“Mshukiwa mkuu, Tyson Kasesi , anaripotiwa kumshambulia afisa wa polisi mnamo Mei mwaka wa elfu mbili ishirini na nne. Afisa huyo alidhulumiwa akiwa kazini kiasi cha kumfanya auguze majeraha kulingana na wajibu wa fomu ya p3 iliyotolewa mahakamani.” Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka ya umma ilidokeza.

Awali Kasesi alikataa kujibu mashtaka kwa nyakati mbili tofauti kabla ya kukiri mashtaka yote manne aliyokabiliwa nayo, mbele ya hakimu mkuu wa Kakamega J.J. Masiga.

Timu ya mashtaka ikiongozwa na Moraa Atandi iliirai mahakama kumpa mshukiwa kifungo kifupi kwa mujibu wa sheria na kanuni.

Akitoa hukumu hiyo, hakimu alibainisha kuwa kosa la kuwashambulia askari polisi linazidi kukithiri nchini hivyo basi adhabu ya kifungo ndiyo inafaa zaidi kwa madhumuni ya kuzuia jamii na mtu yeyote anayekusudia kutenda kosa hilo,” alisema ODPP.

Hukumu hii inajiri siku mbili baada ya kijana wa umri wa miaka 19 kukamatwa kwa kumpiga na kumjeruhi afisa wa polisi wa trafiki huko Mirema. Mshukiwa huyo, Ian Njoroge, alikamatwa nyumbani kwa wazazi wake eneo la Jacaranda, Kayole, Nairobi Jumapili jioni kama sehemu ya oparesheni iliyoongozwa na maafisa wa upelelezi, DCI, jijini Nairobi.

Njoroge alishtakiwa kwa wizi wa mabavu, shambulio lililosababisha madhara makubwa ya mwili na kukataa kukamatwa Jumanne. Wakifika mbele ya Hakimu BenMark katika mahakama ya Milimani, Duncan Okatch na Vincent Lempaa waliambia mahakama kuwa Njoroge, alidhulumiwa nyumbani kwake wakati wa kukamatwa.

Video fupi inayoonyesha Njoroge akihojiwa pia ilichezwa kortini ambayo upande wa mashtaka ulidai kuwa ni dhibitisho dhahiri shahiri la kudhulumiwa kwake tangu maafisa hao walipomtusi. Njoroge alikana mashtaka dhidi yake.

Baadaye, Mahakama iliruhusu upande wa mashtaka siku moja ya kumzuilia Njoroge katika gereza la Industrial Area.