Pensheni ya Uhuru: Wabunge wataka majibu kutoka Ikulu ya rais

Msemaji wa rais mustaafu Kanze Dena alifichua kuwa ofisi hiyo haijakuwa ikipokea ufadhili wake kama inavyotakikana kikatiba.

Muhtasari

• Wabunge wamemtaka msimamizi wa Ikulu Kato Ole Metito kueleza kwa nini afisi ya Aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta imekuwa ikiendeshwa bila ufadhili wa serikali.

Rais mstaafu Uhuru Kenyatta
Rais mstaafu Uhuru Kenyatta
Image: Hisani

Wabunge wamemtaka msimamizi wa Ikulu Kato Ole Metito kueleza kwa nini afisi ya Aliyekuwa Rais Uhuru Kenyatta imekuwa ikiendeshwa bila ufadhili wa serikali.

“Tunawaagiza makarani wetu kumwandikia Msimamizi wa Ikulu kuja na kufika mbele ya kamati kuhusu ni kwa nini afisi ya aliyekuwa rais haipokei fedha zake,” Mwenyekiti wa Kamati ya Utekelezaji Raphael Wanjala alisema Jumanne.

Kamati hiyo ilibainisha kwa masikitiko madai ya Msemaji wa Ofisi ya Rais wa Nne Kanze Dena ambayo yalionyesha kuwa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta amekuwa akifadhili afisi yake rasmi kutoka mfuko wake.

"Hatutaruhusu hilo kutendeka na ilhali tunatenga pesa kama Bunge," aliongeza Wanjala.

Ingawa haijabainika ni lini msimamizi wa ikulu atafika mbele ya kamati ya bunge ya utekelezwaji , wabunge wanataka maafisa hao hao wa Ikulu kufika mbele yao ili kuhakikisha fedha zilizotengwa zinapatikana kwa ajili ya Rais mstaafu.

Siku ya Jumatatu msemaji wa ofisi ya rais wa nne wa Kenya, Kanze Dena alifichua kuwa ofisi hiyo haijakuwa ikipokea ufadhili wake kama inavyotakikana kikatiba.

Kanze alisema kwamba licha ya pesa za matumizi ya ofisi hiyo kuidhinishwa na bunge hawajapokea pesa hizo kwa mwaka wa pili mfululizo.

Pia alidai kuwa serikali imepuuza ombi la kumnunulia rais mustaafu Uhuru Kenyatta magari mapya kama inavyotakikana kikatiba.