Barazala la wanahabari Kenya (MCK) lalaani unyanyasaji wa waandishi

Mkurugenzi Mtendaji wa MCK David Omwoyo alisema polisi waliojihami, ambao walipaswa kuwalinda wanahabari hao sio kuwashambulia.

Muhtasari

• Omwoyo alibaini kuwa wanahabari wasiopungua 5 walishambuliwa na kukamatwa bila ya sababu za msingi.

Mkurugenzi mkuu wa MCK, David Omwoyo
Image: MCK (Facebook)

Baraza la Vyombo vya Habari nchini (MCK) limewasuta polisi kufuatia visa vya unyanyasaji na kukamatwa kwa waandishi wa habari waliokuwa wakiripoti maandamano ya kupinga Muswada tata wa Fedha wa 2024 mjini nairobi

Mkurugenzi Mtendaji wa MCK David Omwoyo alitaja mashambulizi ya maafisa wa polisi waliojihami, ambao walipaswa kuwalinda wanahabari hao, kuwa hayafai kwa vile wanahabari wanaume na wanawake walijitambulisha vya kutosha kwa kutumia beji na jaketi zao za vyombo vya habari .

Aliendelea kuwabaini waandishi wa habari wasiopungua watano ambao walishambuliwa na kukamatwa bila ya sababu za msingi wakiwa katika majukumu yao kwenye maandamano ya ‘Occupy Parliament’, huku kati yao wawili kutoka vyombo vya habari vya kimataifa na watatu wakiwa kwenye vyombo vya habari vya ndani.