Wadukuzi kwa jina 'Anonymous' waonya Ruto na wabunge dhidi ya kupitisha Mswada wa Fedha 2024

Kikundi hicho kilionya kwamba kutokana na nambari za simu za wabunge kuenezwa hadharani, siri zao zinaweza kufichuliwa karibuni.

Muhtasari

•"Imekuja kwa makuwazo yetu kwamba kuna majadiliano bungeni ya kuidhinisha Mswada wa Fedha, ambao utawatoza kodi kiholela raia wa Kenya," walieleza.

• Juhudi za wakenya za kufanya maandamano ya amani dhidi ya mswada huo zimekumbana na unyanyasaji na kukamatwa na polisi.

•Walieleza kwamba wakenya wengi, hawataki Mswada wa Fedha ubadilishwe badala yake, wanataka wabunge waupinge kikamilifu na upesi

Mdakuzi Anonymous
Image: HISANI

Kikundi cha kimataifa cha wadukuzi na waandamanaji, Anonymous, kimetoa onyo kwa wabunge wa Kenya kuhusu kuidhinishwa kwa Mswada wa Fedha wa mwaka 2024.

Katika ujumbe uliosambazwa kwenye akaunti yao rasmi ya X, kikundi hicho cha wadukuzi kilisema kwamba wamebaini kuwa wabunge wanataka kuidhinisha mswada ambao utawatoza kodi nzito wananchi wa Kenya.

"Imekuja kwa makuwazo yetu kwamba kuna majadiliano bungeni ya kuidhinisha Mswada wa Fedha, ambao utawatoza kodi kiholela raia wa Kenya," walieleza.

Anonymous alisema kuwa, juhudi za wakenya za kufanya maandamano ya amani dhidi ya mswada huo zimekumbana na unyanyasaji na kukamatwa na polisi.

Kikundi hicho kilionya kwamba kutokana na nambari za simu za baadhi ya wabunge kuenezwa hadharani, siri zao zinaweza kufichuliwa hivi karibuni.

"Kwa bahati nzuri, nambari za simu za baadhi ya wabunge zinasambaa mtandaoni. Hivi karibuni, kutakuwa na vuguvugu la wadukuzi,ambao wengi wao wanaweza kuwa wanaishi katika nchi yenu.”

"Siri zenu huenda sasa haziko salama, na kuna nafasi kwamba siri zote hizi zitafichuliwa."

Walieleza kwamba wakenya wengi, hawataki Mswada wa Fedha ubadilishwe badala yake, wanataka wabunge waupinge kikamilifu na upesi.

Anonymous aliwasihi wabunge kusikiliza vilio vya wakenya.

"Alhamisi, tarehe 20 Juni, Wakenya wataandamana na kauli mbiu #OccupyParliament. Hatutaki mubadilishe Mswada wa Fedha; tunataka muiukatae. Sikilizeni vilio vya wananchi wenu, au watu wa dunia wataupinga kila hatua mnayochukua. Wananchi wa Kenya, msiwe na wasiwasi, Tuko Pamoja," kikundi hicho kilisema.

 

Onyo hilo limekuja huku Ofisi ya Kamishna wa Ulinzi wa Data Jumatano ikiwaonya wakenya dhidi ya kusambaza taarifa za kibinafsi za watu hadharani.

Katika taarifa, Kamishna wa Data alisema kuwa sehemu ya wakenya waliotenda hivyo wamekiuka kipengee cha 31 ya Katiba.

"Tabia hii imekuwa ikifanyika bila idhini ya raia walioathirika kinyume na matakwa ya kipengee 31 cha katiba ya Kenya, Sheria ya Ulinzi wa Data ya mwaka 2019 na kanuni zake zinazohusiana.

"Kwa kuzingatia yaliyotangulia, ofisi inapenda kushauri umma kujizuia kusambaza taarifa za kibinafsi zinazokiuka haki za faragha za watu binafsi," ofisi ilisema hivyo.

Vilevile, liongeza kwamba baadhi ya taarifa ambazo zimesambazwa bila idhini ni pamoja na majina, nambari za simu, maeneo na maelezo ya familia za waathiriwa.

Kamishna wa Data pia aliwaomba wale ambao taarifa zao zimesambazwa kufungua malalamiko.