IPOA kuchunguza kifo cha Rex Masai na waathiriwa wengine wa maandamano

Rex aliaga kutokana na kufuja damu nyingi mwilini

Muhtasari

•Mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia tabia ya polisi tangu kuanza kwa maandamano mnamo Jumanne.

• Rex Kanyike alipigwa risasi na polisi akiwa njiani akirudi nyumbani mnamo saa saba usiku akiwa na sahibu yake wa ndani nje ya mkahawa wa Hilton

Kijana aliyepigwa risasi na kufariki Rex Masai
Image: MAKTABA

Mamlaka huru ya kudhibiti shughuli za Polisi (IPOA) imeanzisha uchunguzi kuhusu kifo cha Rex Kanyike Masai, kijana wa miaka 24 aliyedaiwa kuuawa na polisi jijini Nairobi Alhamisi wakati wa maandamano dhidi ya mswada wa kifedha.

Katika taarifa ya X, mwenyekiti wa IPOA Anne Makori, akitoa pole kwa familia ya marehemu, alisisitiza kuwa mamlaka hiyo imekuwa ikifuatilia tabia ya polisi tangu kuanza kwa maandamano mnamo Jumanne.

Vilevile, Makori aliongezea kuwa wakati wa maandamano, waandamanaji na polisi kwa ujumla walionyesha kijizuia dhidi ya vurugu na vurumai.

Hata hivyo, alinyoshea kidole matukio maalum hasa kesi ya Masai na majeraha yaliyopatikana kwa waandamanaji wengine wakati wa pilkapilka hiyo ya maandamano.

"Taarifa za awali zinaonyesha kuwa Rex Kanyike alipigwa risasi na polisi akiwa njiani akirudi nyumbani mnamo saa saba usiku akiwa na sahibu yake wa ndani nje ya mkahawa wa Hilton kando ya barabara ya Moi Avenue," alisema Makori.

"Risasi hiyo ilisalia kwenye mwili wake na hatimaye kusababisha kifo cha Rex ambacho kilitokana na kufuja damu nyingi kutoka mwilini," aliongeza.

Imeelezwa kuwa alitumia zaidi ya dakika takriban 20 kujaribu kutafuta matibabu kabla ya kupelekwa haraka upesi katika kituo cha matibabu cha Bliss kando ya barabara ya Moi Avenue ambapo alithibitishwa kufariki alipowasili.