Jinsi nguvu ya vijana wa Gen Z ilivyomlazimu rais wa Kenya kunyenyekea

Ruto alisema serikali ilifanya maamuzi magumu ili kuleta utulivu wa uchumi na kusaidia kuinasua Kenya kutoka kwenye mtego wa madeni.

Muhtasari

• Badala ya kuongeza mapato ya ziada, Bw Ruto sasa ananuia kusawazisha vitabu kwa kuanzisha mpango mpya wa kubana matumizi ya Umma.

Matukio ambayo yalisababisha William Ruto kuachana na bajeti yake huenda baadaye yakaonekana kama wakati muhimu, sio tu kwa rais wa Kenya lakini pia kwa nguvu ya vijana katika bara changa zaidi duniani.

Kupitia nguvu ya maandamano, yaliyoandaliwa kwa kiasi kikubwa , vuguvugu lililoanzishwa na vijana kwenye mitandao ya kijamii limemlazimu mmoja wa viongozi wanaotambulika kimataifa barani Afrika kubadili sera yake ya uongozi.

Si kwamba Bw Ruto sasa anatambua kuwa alikuwa amekosea kushinikiza nyongeza ya ushuru ambayo ilizua hasira nyingi kote nchini Kenya. Kwa hakika alianza hotuba yake kwa taifa siku ya Jumatano kwa maelezo thabiti na ya kina ya kwa nini aliamini yalihitajika.

Serikali yake, alisema, ilifanya maamuzi magumu muhimu ili kuleta utulivu wa uchumi na kusaidia kuinasua Kenya kutoka kwenye mtego wa madeni ambao unailazimu kutumia senti 61 ya kila dola ya ushuru katika kulipa mikopo yake.

Muswada wa fedha ulikuwa muhimu, alidai, "kukomboa nchi yetu kutoka kwenye usumbufu wa deni na kusisitiza uhuru wetu".

Hilo linashangaza zaidi kwamba msukosuko wa siku za hivi karibuni umemlazimu rais huyo kubadili mwelekeo kabisa.

Badala ya kuongeza mapato ya ziada, Bw Ruto sasa ananuia kusawazisha vitabu kwa kuanzisha mpango mpya wa kubana matumizi ya Umma.

Itakuwa ni pamoja na kupunguza matumizi katika ofisi yake mwenyewe, ishara ya wazi ya hasira iliyosikika kutoka kwa wengi mitaani kuhusu ufisadi katika serikali.

Na katika kujaribu kuwafikia moja kwa moja vijana wa Kenya, rais aliahidi kuwashirikisha na kuwasikiliza.

Bw.Ruto alizungumza mbele ya hadhara ya wabunge wake, ambao aliwashukuru kwa kuunga mkono muswada wake. Wengi wanaweza sasa kusamehewa kwa kujiuliza mabadiliko hayo yanauweka wapi uaminifu wao.

Hakuna shaka kwamba siku mbili zilizopita zimekuwa za changamoto kali kwa rais.

Vikosi vyake vya usalama vililaaniwa vikali kwa kuchukua hatua za kikatili kwenye maandamano ya Jumanne ambapo takribani watu 22 wanaripotiwa kufariki, wengine kadhaa wakipigwa risasi na polisi.

Mara tu baada ya maandamano hayo ya umwagaji damu, Bw Ruto aliangazia uhalifu uliokithiri katika kiini cha machafuko hayo, na kutishia kukabiliana kwa nguvu na mashambulizi dhidi ya bunge na uporaji mkubwa.

Lakini makubaliano yake kuhusu kiini cha sera yake siku ya Jumatano yalikuja pia kwa kukubali kwamba maandamano yalikuwa moyoni yalikuwa ishara ya hasira.

"Imedhihirika," alikiri, "kwamba Umma bado unasisitiza juu ya hitaji la sisi kufanya makubaliano zaidi".

"Ninaendesha serikali, lakini pia ninaongoza watu, na watu wamezungumza."

Baadhi wameitisha maandamano yaliyopangwa siku ya Alhamisi kuendelea, wakitaka rais ajiuzulu.

Siku zijazo zitaonesha ikiwa zimwi la ghadhabu ya umma linaweza kurejeshwa kwenye chupa.

Zaidi ya Kenya, Bw Ruto atakuwa anashangaa jinsi mgogoro huo umeathiri hadhi yake duniani.

Baadhi ya washirika wa karibu wa kidiplomasia wa nchi yake na katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa waliitaka Kenya kudumisha haki ya maandamano ya amani ya umma.

Shinikizo hilo linaweza kuwa lilichangia katika tofauti ya sauti kati ya hotuba zake Jumanne na Jumatano.

Pengine pingamizi kwa ghasia zilizooneshwa na maafisa wake wa usalama litakuwa na nguvu katika kuchagiza jibu la Bw Ruto kama vile kuonekana kwa maelfu ya watu wakiandamana dhidi yake.

Chochote kilichosababisha hatua yake mpya, chini ya miaka miwili katika uongozi wake, kazi sasa kwa Bw Ruto ni kujenga upya na kurejesha kasi.

Lakini rais wa Kenya ameachwa kufuata sera ya kiuchumi ambayo haonekani kuiamini.

Huenda baadhi ya wapinzani wa Bw.Ruto wakauona ujumbe wa jana kama kauli yenye nia na funzo ambalo limemlazimu kiongozi kuwa mnyenyekevu.

Lakini kwa wengine ushindi huu dhidi ya mtawala mwenye nguvu unaweza kutoa msukumo mpya kuendelea kupinga utawala wake.

Na kipindi hiki kinaweza kusikika kwingineko barani Afrika pia.

Kwa sababu ingawa zamu ya Bw Ruto ilichochewa na zaidi ya hasira ya vijana, alijitambua kuwa ni vijana wa Kenya waliochochea moto huo.

Kama bara, Afrika ina idadi ndogo zaidi ya watu duniani, ikiwa na karibu robo tatu ya raia chini ya miaka 35.

Wengi wao wataona matukio ya Jumatano kama uthibitisho kwamba kwa dhamira ya kutosha, wanaweza kuwalazimisha viongozi wao kusikia sauti zao.