Dennis Itumbi ajawa bashasha baada ya kuwabwaga chini wadukuzi

CAS huyo alibainisha kwamba wadukuzi hao watatatizika sana kupata akaunti yake tena.

Muhtasari

•Akaunti hiyo yenye wafuasi zaidi ya milioni mbili ilikuwa imedukuliwa kwa takriban wiki mbili na wauzaji wa crypto.

•Itumbi alibainisha kuwa wadukuzi hao pia walijaribu kudhibiti akaunti zake nyingine za mitandao ya kijamii .

Image: FACEBOOK// DENNIS ITUMBI

Katibu Mwandamizi katika wizara ya Teknolojia, Habari na Mawasiliano, Dennis Itumbi amejawa na bashasha baada ya kurejesha akaunti yake ya Twitter.

Akaunti hiyo yenye wafuasi zaidi ya milioni mbili ilikuwa imedukuliwa kwa takriban wiki mbili na wauzaji wa crypto.

Akizungumza baada ya kufanikiwa kuirejesha, Itumbi alisema kwamba amewabwaga chini wadukuzi hao.

Mwanahabari huyo alibainisha kwamba wadukuzi hao watatatizika sana kupata akaunti yake tena.

"Niliwashinda Wadukuzi - Waliweza kunifungia nje kwa muda. Nilipanda bendera ya ushindi katika eneo lao pia. Watajitahidi kurejea.Usiku mwema watu," Itumbi alisema Jumanne.

Akizungumza baada ya akaunti yake kudukuliwa wiki mbili zilizopita, alieleza imani kwamba angechukua udhibiti wa akaunti hiyo baada ya muda mfupi.

Itumbi alibainisha kuwa wadukuzi hao pia walijaribu kudhibiti akaunti zake nyingine za mitandao ya kijamii lakini aligundua kabla hawajaweza.

"Kuhusu akaunti yangu, itarejeshwa hivi karibuni, walijaribu barua pepe yangu, Instagram na Facebook pia, lakini nilipata kabla hawajaweza. Kukaribishwa kwa kikatili na ujumbe wazi juu ya Usalama wa Mtandao. Kwa sasa Hackers 1 - Itumbi 0. Katika ukamilifu wa muda, alama hiyo itakuwa kitu kingine... Asanteni," alisema.

Itumbi alisema udukuzi huo unapaswa kuwa ujumbe wazi juu ya kile kinachofaa kufanywa kuhusiana na usalama wa mtandao nchini Kenya.